1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Syria waendelea kushambuliwa Aleppo

Daniel Gakuba
28 Septemba 2016

Jeshi la Syria limeendeleza mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi mjini Aleppo na kuharibu magari yao ya kijeshi. Benki ya dunia imetoa dola milioni 300 kuwasaidia wakimbizi wa Syria waishio Jordan.

https://p.dw.com/p/2QgRW
Syrien Armee erobert Teile von Aleppo
Picha: picture alliance /abaca/M. Sultan

Taarifa hizo za mashambulizi yanayoendelea kuwalenga waasi katika mji wa Aleppo na viunga vyake zimethibitishwa na jeshi la Serikali ya Syria, ambalo limesema katika taarifa yake kwamba limeyaharibu magari ya kivita ya waasi hao, baadhi yakiwa yamebeba bunduki za rashasha.

Ripoti zaidi zimesema hospitali iliyo Mashariki mwa Aleppo imeharibiwa kabisa na makombora yaliyorushwa na ndege yakiilenga moja kwa moja hospitali hiyo. Daktari mmoja katika hospitali hiyo ya M10 Mohammed Abu Rajab, amesema vipande vya nyumba vilivyobolewa na makombora hayo vimewaangukia wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika wadi ya wagonjwa mahtuti.

Tangu kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mashambulizi wiki iliyopita, maeneo yaliyo chini ya udhibiti mjini Aleppo yamekuwa yakishambuliwa vikali, hali iliyozusha wasiwasi miongoni mwa jumuiya ya kimataifa, kuhusu majaliwa ya watu zaidi ya 250,000 waishio katika maeneo hayo.

Hakuna muda wa kupumua

Syrien Aleppo Männer in Trümmern mit Säuglingen
Wakazi 250,000 wa mji wa Aleppo wanaishi katika mashaka makubwaPicha: Getty Images/AFP/A. Alhalbi

Mkuu wa kundi la waasi la Syria Civil Defence, Raed al-Saleh, amesema kwa muda sasa hawajaweza kupumua kutokana na mfululizo wa mashambulizi hayo.

''Mnamo siku nane zilizopita mji wa Aleppo umeshuhudia mashambulizi makali kabisa. Tumerekodi mashambulizi ya anga yasiopungua 1700. Kumi na saba kati ya mashambulizi hayo, yalikuwa yenye nguvu za kuvunja majengo makubwa'',  amesema kiongozi huyo wa waasi na kuongeza kwamba  mashambulizi mengine 200 yalikuwa ya mabomu ya mtawanyiko na silaha nyingine ambazo zimepigwa marufuku kimataifa.

Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lililo na makao yake nchini Uingereza, limesema kiwanda cha kuoka mikate katika mtaa wa al-Maadi pia kimeshambuliwa kwa mizinga, ambayo imuuwa watu sita waliokuwepo.

Huku hayo yakijiri, juhudi za kuwasaidia wasyria walikimbia vita zinaendelea. Benki ya Dunia imetangaza mpango wenye thamani ya dila milioni 300, ambao utawasaidia wakimbizi wa Syria waishio nchini Jordan kupata fursa katika soko la ajira.

Wakimbizi wasaidiwa kujitegemea

Mkuu wa Benki ya Dunia katika eneo la Mashariki ya Kati Ferid Berhaj amesema fedha hizo zitasaidia kuwahamasisha wawekezaji wanaoweza kuwashirikisha wakimbizi kutoka Syria, ili waweze kujikimu kimaisha na kuchangia katika uchumi wa nchi iliyowapokea, badala ya kuendelea kutegemea tu msaada wa kiutu.

Junge hält Hilfsgüter die über einen Kran über die jordanisch syrische Grenze gebracht wurden
Lengo ni kuwasaidia wakimbizi kujikimu badala ya kutegemea msaadaPicha: picture-alliance/AP Photo/Malleruzzo

Hali kadhalika juhudi za kidiplomasia hazijasitishwa. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Javad Zarif amefanya ziara nchini Uturuki kuzungumza na maafisa wakuu wa nchi hiyo, mzozo wa Syria ukiwa miongoni mwa mada za mazungumzo yao.

Ingawa Iran na Uturuki zinaunga mkono pande zinazokinzana katika vita vya Syria, hii ni ziara ya tatu ya Zarif nchini Uturuki katika muda usiozidi wiki sita.

Uturuki inataka kuundwa kwa kile kinachoitwa ''eneo salama'' Kaskazini mwa Syria kwa ajili ya wakimbizi wanaoikimbia nchi hiyo. Pendekezo hilo linatiliwa mashaka na pande tofauti duniani, ikiwemo serikali ya Ujerumani ambayo wasiwasi wake ulielezwa na Kansela Angela Merkel hapo jana.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga