1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Ethiopia wanasema serikali haiwezi 'kuaminiwa'

Saleh Mwanamilongo
24 Juni 2022

Kundi la waasi la Ethiopia, Ijumaa, liliitisha uchunguzi huru kuhusu mauaji ya watu wengi magharibi mwa nchi, likisema kuwa serikali haiwezi kuaminiwa kufanya uchunguzi bila upendeleo

https://p.dw.com/p/4DDAC
Äthiopien | Mekele | Verwundete äthiopische Gefangene im Mekele Rehabilitation Center
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Mkuu wa Tume ya haki za binabamu ya Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet siku ya Alhamisi alizitaka mamlaka za Ethiopia kufanya uchunguzi "wa haraka, usio na upendeleo na wa kina" kuhusu mashambulizi ya mwishoni mwa juma lililopita katika eneo la Oromia ambayo yameripotiwa kupoteza maisha ya mamia ya watu, wengi wao wakiwa wa kabila la Amhara.

"Mamlaka ya Ethiopia haiwezi kuaminiwa kufanya uchunguzi bila upendeleo," Odaa Tarbii, msemaji wa waasi wa Oromo Liberation Army (OLA), aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

Serikali ya Addis Ababa na mamlaka za kikanda huko Oromia wamelilaumu kundi la OLA, ambalo serikali imelitaja kuwa kundi la kigaidi, kwa mauaji katika kijiji cha Tole. Lakini kundi la waasi, ambalo linashirikiana na Kundi la Ukombozi wa Watu wa Tigray, (TPLF) katika vita vyake dhidi ya vikosi vya serikali kaskazini mwa Ethiopia, limewalaumu wanamgambo wanaoiunga mkono serikali katika eneo la Oromia.

Walionusurika na shambulio la Tole wameliambia shirika la habari la AFP kwamba mamia ya watu wa kabila la Amhara waliuawa na waasi, huku maiti zikiwa bado zimetapakaa mitaani baada ya saa kadhaa za ghasia.

Soma pia→Watu milioni 20 nchini Ethiopia wanakabiliwa na baa la njaa

Uchunguzi wa kimataifa ?

Watu wasiopungua 2,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao
Watu wasiopungua 2,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yaoPicha: Efratana Gidm woreda Communication

Bachelet alisema Alhamisi kuwa wafanyakazi wake walizungumza na mashahidi wa mauaji ya Juni 18 ambao walisema watu wenye silaha walifika Tole na kuanza kufyatua risasi ovyo, na kuwauwa mamia ya watu. Wengi wa waathiriwa walikuwa wanawake na watoto, taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema, ikiongeza kuwa watu wengine wasiopungua 2,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Serikali haijatangaza idadi rasmi ya machafuko hayo. Chama cha Amhara chenye makao makuu yake nchini Marekani kilisema katika ripoti yake kuwa kimewatambua waathiriwa 282, lakini wakaongeza kuwa idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi. Mwathiriwa mkubwa anayejulikana, ilisema, alikuwa mzee wa miaka 100, na mdogo zaidi mtoto wa mwezi mmoja. Idadi hiyo ya waathirika haikuweza kuthibitishwa na duru isiyopendelea upande wowote.

Soma pia→UN: Zaidi ya watu 300 wameuawa Ethiopia tangu Novemba

Siku ya Alhamisi, bunge la nchi hiyo liliiagiza Tume ya Haki za Kibinadamu ya Ethiopia, chombo huru chenye uhusiano na serikali, kuchunguza "ukatili usio wa kibinadamu" uliotekelezwa na OLA huko Oromia, pamoja na eneo jirani la Gambella.

Shirika la haki za binadamu la Ethiopia, EHRC, wiki iliyopita ilisema kwamba vikosi vya usalama viliwanyonga wakazi katika mji mkuu wa mkoa wa Gambella, wakiwashuku kwa kushirikiana na waasi wa OLA ambao hapo awali waliushambulia mji wa kusini magharibi mwa jimbo hilo.