Waasi: Syria yapeleka silaha za kemikali mipakani
24 Julai 2012Brigedia Qassim Sa'addin wa Jeshi Huru la Syria, amekiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera mapema leo kwamba wana uhakika kwamba silaha za kemikali za Syria zimepelekwa maeneo ya mpakani.
Kiongozi huyo wa waasi, ambaye kabla ya kujiunga na upinzani alikuwa mwanajeshi wa ngazi za juu kwenye jeshi la Syria, amesema baadhi ya silaha hizo pamoja na vifaa vya kuchanganyia kemikali vimewekwa kwenye viwanja vya ndege karibu na mpaka kwa lengo la kuitisha jumuiya ya kimataifa..
Kauli ya jana ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria, Jihad Maqdis, kwamba serikali yake haitatumia silaha za kikemikali dhidi ya watu wake, bali kwa wachokozi wa nje tu, ilizua lawama kubwa za kimataifa, huku Rais Barack Obama wa Marekani, akiionya Syria isije ikafanya kile alichokiita "kosa la kuhuzunisha.":
"Hivi sasa ulimwengu unalifanyia kazi suala la kipindi cha mpito nchini Syria, ili Wasyria wawe na mustakabali mwema, wakiwa huru na utawala wa Assad. Na kuhusu suala la kauli ya utawala huo ya matumizi ya silaha za kemikali tutaendelea kusema wazi kwa Assad na wale waliomzunguka, kwamba dunia inawatazama na kwamba watabebeshwa dhamana na jumuiya ya kimataifa na Marekani, ikiwa watafanya kosa la kuhuzunisha la kutumia silaha hizo." Amesema Obama.
Waasi wafanikiwa kuteka wilaya za Allepo
Hata hivyo, televisheni ya nchi hiyo hivi leo imepunguza makali ya kauli ya Maqdis, ikimnukuu katika kauli mpya akisema kwamba "kamwe Syria haitatumia silaha za kikemikali na kibailojia, na silaha kama hizo kama zipo, ni kawaida kuhifadhiwa na kuwa salama."
Hayo yanaripotiwa katika wakati ambapo waasi wamefanikiwa kuzichukuwa wilaya kadhaa za mji wa kaskazini wa Allepo. Shirika la Haki za Binaadamu la Syria limesema kumetokea uasi kwenye gereza kuu la mji huo, ambapo wafungwa saba wameuawa na wengine 16 kujeruhiwa.
Jeshi Huru la Syria limeuelezea uasi huo kama hatua ya kwanza kuelelekea ukombozi kamili wa mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Syria. Lakini televisheni ya serikali imeripoti kwamba usiku wa jana ulikuwa ni wa nne wa mapigano makali, ambapo wanajeshi wa serikali wamewashinda waasi katika wilaya za Salaheddine na Sukkari.
Waasi tayari kuongozwa na mfuasi wa Assad
Katika hatua nyengine, Baraza la Kitaifa la Syria, ambalo ni tawi la kisiasa la waasi, limesema liko tayari kukubali kipindi cha mpito kitakachoongozwa kwa muda na mjumbe kutoka utawala wa Rais Assad.
Akizungumza na shirika la habari la AFP hivi leo, msemaji wa Baraza hilo, Georges Sabra, amesema watakubaliana "na kuondoka kwa Assad na kukabidhi madaraka kwa mtu mwengine kuendesha kipindi cha mpito, kama ilivyotokea kwa Yemen."
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil El-Arabi, amesema siku za utawala wa Assad zinahesabika. Katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti la al-Hayat, El-Arabi amesema "wakati wa mageuzi ya kisiasa umemalizika na sasa ni wakati wa kukabidhi madaraka."
Kauli kama hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, aliyesema hivi sasa wimbi la mageuzi ya Syria linakaribia sana kwenye ushindi kuliko wakati mwengine wowote huko nyuma. Uturuki ni miongoni mwa majirani wa Syria ambao wamemtaka wazi Assad ajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza wito wa mageuzi, huku maelfu ya watu wakipoteza maisha na wengine kukimbilia nchini humo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPDPAReuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman