Waangola wapiga kura
1 Septemba 2012Vingi kati ya vituo 10,000 vya kupigia kura vilivyowekwa katika maeneo ya shule nchi nzima, vilifungwa katika muda muda uliopangwa na zoezi la kuhesabu kura lilianza mara moja.Maafisa wa tume ya uchaguzi wamesema kuwa baadhi ya vituo vya kupigia kura vilibaki wazi kwa muda , bila ya kutoa maelezo zaidi.
Uchaguzi huo umekumbwa na matatizo machache hapa na pale, lakini ni uchaguzi ambao umefanyika kwa mafanikio makubwa ikilinganishwa na uchaguzi uliofanyika mwaka 2008 wakati uchaguzi huo ulihitaji kurefushwa hadi siku ya pili kutokana na mtafaruku katika vituo vya kupigia kura.
Uchaguzi ulienda vizuri
Pedro Verona Pires , mkuu wa kundi la wachunguzi wa uchaguzi kutoka umoja wa Afrika, ameueleza utayarishaji wa uchaguzi huo kuwa wa kuridhisha, akiongeza kuwa hali ya upigaji kura ilikuwa nzuri.
"Kila mmoja anakubali kuwa uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa umetayarishwa vizuri zaidi kuliko mwaka 2008," Pires , ambaye pia ni rais wa zamani wa Cape Verde ameliambia shirika la habari la AFP.
UNITA kimeonyesha wasi wasi
Chama cha upinzani cha UNITA kimeeleza wasi wasi wake kuwa waungaji wake mkono wasingekubaliwa kupiga kura kutokana na matatizo katika daftari la wapiga kura, wakati baadhi ya wachunguzi wao wa uchaguzi hawakuruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura.
Wapiga kura walikuwa wanawachagua wabunge katika bunge lenye wajumbe 220 nchini humo. Kiongozi wa chama ambacho kitapata kura nyingi moja kwa moja anakuwa kiongozi wa nchi. Hakuna shaka kwamba Dos Santos atafanikiwa kurejea madarakani na kuendelea na uongozi wa nchi hiyo alioshikilia kwa muda wa miaka 33 sasa.
Chama chake cha People's Movement for the Liberation of Angola, MPLA kilipata zaidi ya asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa mwaka 2008, uchaguzi ambao ulionekana kuwa ni halali na baadhi ya wachunguzi licha ya matatizo kadha katika vituo vya uchaguzi. Dos Santos ametumia miongo kadha akiwa kiongozi wa nchi hiyo kuweka madaraka mikononi mwake. Familia yake hususan mwanawe wa kike Isabel, ametumia utajiri mkubwa wa mafuta nchini Angola kujenga himaya ya kibiashara ya kimataifa.
Ujenzi mpya
Pia amemimina mabilioni ya dola katika kuijenga upya Angola baada ya miaka 41 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa ni pamoja na miaka 14 ya mapambano ya ukombozi dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ureno na hatimaye kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa miaka 27 baada ya uhuru mwaka 1975. Ametumia udhibiti wake katika vyombo vya habari vya taifa kuonyesha mabarabara , mabwawa ya kufua umeme, mashulre na zahanati vilivyojengwa tangu mapigano yalipomalizika muongo mmoja uliopita.
Maisha nchini Angola kwa kiasi kikubwa yamekuwa bora. Uchumi katika muda wa muongo mmoja uliopita umekuwa miongoni mwa uchumi unaokuwa kwa kasi kabisa duniani. Pato jumla la taifa kwa mwaka limefikia karibu dola bilioni 1.9 katika mwaka 2009, na kuchupa mara tatu kutoka ukuaji mwaka 2000. Matarajio ya maisha ya watu yamepanda kutoka kiasi cha miaka 40 mwaka 1980 na kufikia kiasi cha miaka 51 hivi sasa.
Matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa Jumamosi mchana (01.09.2012), amesema mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi. Matokeo kamili yanatarajiwa kutolewa wiki ijayo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Idd Ismail Ssessanga