1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji waondoka eneo la ubalozi wa Marekani, Baghdad

Sekione Kitojo
2 Januari 2020

Waungaji mkono wa makundi ya kijeshi nchini  Iraq yanayoungwa mkono na Iran ambao walivamia maeneo ya viunga vya ubalozi wa  Marekani na kurusha mawe katika maandamano ya siku mbili wameondoka jana(01.01.2020).

https://p.dw.com/p/3Vaon
Irak l Proteste bei der US-Botschaft in Bagdad
Picha: Reuters/T. al-Sudani

Hatua  hiyo  imewezekana  baada  ya  Marekani kupeleka  vikosi vya  ziada na  kutishia  kuchukua  hatua  dhidi  ya  Iran. Lakini  wachambuzi wa masuala  ya  kisiasa  wanaonya  kuwa  hali  hiyo  inaweza  kuwa  na athari  za  kudumu  katika  sekta tete  ya  usalama  nchini  Iraq pamoja  na  mahusiano  ya  kidiplomasia.

Irak l  Proteste und Angriffe auf die US-Botschaft in Bagdad
Waandamanaji wakipambana na vikosi vya Marekani mjini BaghdadPicha: picture-alliance/AP/K. Mohammed

Waandamanaji , ambao wamekasirishwa  na  mashambulizi  ya anga  ya   vikosi  vya  jeshi  la  Marekani  dhidi  ya  kundi linaloungwa  mkonom na  Iran  la  Hezbollah  ambapo  kiasi  ya  watu 25 waliuwawa, walirusha  mawe katika  jengo  la  ubalozi  wakati wanajeshi wa   jeshi  la  Marekani  waliokuwa  katika  mapaa ya jengo  hilo  wakifyatua  mabomu  ya  kutoa  machozi kuwatawanya.

Ilipofika  mchana , wengi walionekana  kutii wito  wa  kujiondoa kutoka  katika  eneo  hilo, uliotolewa  na  kundi  la  wanamgambo  wa Kishia linaloongoza  vikundi  vya umma  vya  mapambano PMF, ambalo  lilisema  ujumbe  wa  waandamanaji  tayari  umesikika.

Vijana walitumia  matawi  ya miti  ya  mitende kufajia  mtaa  mbele ya  eneo  la  ubalozi  wa  Marekani. Wengine  walikusanya  vifaa hivyo na magari yaliwasili  kuvichukua.

Trump hataki vita

Maandamano  hayo  yameonesha mabadiliko  mapya  katika  kivuli cha  vita  kati  ya  Marekani  na  Iran  vinavyotokea  katika  eneo  la mashariki  ya  kati. Rais Donald Trump  ambaye  anakabiliwa  na kampeni  ya  uchaguzi  mwaka  2020, ameishutumu  Iran kwa kuchochea  ghasia  hizo. Ametishia  siku  ya  Jumanne  kuchukua hatua  dhidi  ya  iran lakini  alisema  baadaye  kuwa  hataki  vita. Makamu  ya  rais  katika  taasisi  ya  Charles Koch  anayehusika  na utafiti  na  sera Will Ruger  amesema  hatua Marekani  inazochukua kuibinya Iran hazitafanyakazi:

Irak l  Proteste und Angriffe auf die US-Botschaft in Bagdad
Wanajeshi wa Iraq wakilinda wakati wazima moto walijaribu kuuzima moto uliowashwa na wanamgambo na waungaji wao mkono mjini BaghdadPicha: picture-alliance/AP/K. Mohammed

"Moja ya  matatizo  hapa  ni  kwamba  sio tu shambulio la  roketi  la jeshi  la  Marekani ndio lililochochea mzozo  huu, lakini  pia  kile tulichoshuhudia  jana katika  ubalozi wa  Marekani mjini  Baghdad, nafikiri  hii inaonesha  kwamba  kampeni  kubwa  ya  shinikizo ambayo  utawala  wa  Trump  umekuwa  ukitumia dhidi  ya  Inar haifanyikazi kupunguza  wasi  wasi. Na haifanyi Iran kutulia. Badala yake  inaleta  uhasama na  changamoto nyingi kwa  mahusiano."

Iran katika  hali  mbaya ya  kiuchumi

Iran , ikiwa  katika  hali  mbaya  ya  kiuchumi kutokana  na  vikwazo vya  kuumiza  vilivyowekwa  na  Trump, imekana  kuhusika. Ghasia hizo  zilitokana  na  mashambulizi  ya  anga  siku  ya  Jumapili dhidi ya  vituo  vya  kundi  la  Kataib Hezbollah kwa  kulipiza  kisasi  kwa mashambulizi  ya  makombora  ambayo  yalisababisha  kifo  cha mkandarasi  wa  Marekani  kaskazini  mwa  Iraq wiki  iliyopita.

Marekani imesema  wanadiplomasia wako salama na inapeleka  mamia  ya  wanajeshi wa ziad  katika  eneo  hilo. Wizara ya  mambo ya kigeni ya  Marekani imesema  jana  kuwa  waziri wa  mambo  ya  kigeni Mike Pompeo  ameamua  kuahirisha  ziara  yake  kwenda  Ukraine, Belarus , Kazakhstan, Uzbekistan, na  Cyprus  na  kubakia  mjini  Washington ili  kufuatilia  hali  nchini  Iraq.

Mike Pompeo, General Mark Milley und Mark Esper
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo (katikati)Picha: Reuters/T. Brenner

Pompeo alizungumza  jana  Jumatano  na  waziri mkuu  wa  Iraq  Adel Abdul mahdi, emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani  na  waziri  mkuu  wa  Israel Benjamin Netanyahu , wizara  ya  mambo  ya  kigeni  imesema.

Pompeo aliandika  katika  ukurasa  wa  Twitter kuwa  Abdul Mahdi alikubali  kuwa  Iraq "itaendelea  kuheshimu jukumu  lake  la  kuyapa usalama  majeshi  ya  marekani na  kuyaondoa  makundi  yanayoungwa mkono  na  Iran  kuyapeleka  maeneo  ya  mbali.