Waandamanaji Peru wamg'ang'ania rais aondoke
25 Januari 2023Maelfu ya waandamanaji waliomiminika barabarani mjini Lima, wamekabiliwa na maafisa wa polisi kwa kurushiwa gesi ya kutoa machozi saa chache baada ya rais wa Peru, Dina Boluarte kutoa wito wa kitaifa wa usitishwaji uhasama baada ya takriban miezi miwili ya maandamano.
Maandamano ya kuipinga serikali yaliyofanyika jana nchini humo ndio yaliokuwa makubwa na yaliojaa ghasia tangu yale ya siku ya Alhamisi wiki iliyopita, wakati makundi makubwa ya watu wengi kutoka maeneo ya Andean walipomiminika mjini Lima wakitaka rais Boluarte kujiuzulu, kufanyika kwa uchaguzi wa haraka na kuvunjwa kwa bunge.
Waandamanaji wamekasirishwa na kuuwawa kwa zaidi ya wenzao 40 kufuatia machafuko yaliyozuka tangu rais wa zamani Pedro Castillo kuondolewa madarakani kwa nguvu mwezi uliopita kwa madai ya kuhusika na uasi alipojaribu kulivunja bunge.