1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya upinzani kususia uchaguzi Burundi

Admin.WagnerD26 Juni 2015

Vyama vya upinzani nchini Burundi vimetangaza kususia chaguzi zote zijazo, vikisema haitakuwa rahisi uchaguzi kufanyika kwa haki kufuatia wiki kadhaa za vurugu za kupinga jitihada za Nkurunziza kubakia madarakani.

https://p.dw.com/p/1Fnkg
Burundi Proteste gegen Präsident Nkurunziza
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Vyama vyote vya Upinzani vimekuwa na kauli moja na kuamua kususia uchaguzi," ilisema barua iliyosainiwa na wawakilishi wa vyama vyote vya siasa vya upinzani. Uchaguzi wa wabunge na madiwani umepangwa kufanyika siku ya Jumatatu, na ule wa rais utafanyika tarehe 15 Julai.

Nchi hiyo ya Afrika ya Kati ilitumbukia kwenye machafuko mwishoni mwa mwezi April baada ya rais Pierre Nkurunziza kuanzisha kampeni ya kugombea muhula wa tatu. Wapinzani wake wanasema hatua hiyo ni kinyume na katiba na ukiukwaji wa makubaliano ya amani ya Arusha yaliyokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2006.

Barua hiyo ya upinzani, ambayo inaikosoa ratiba pia ratiba iliyotangazwa na tume ya uchaguzi, inasema wapinzani hawatashiriki uchaguzi hadi mazingira yawekwe ya kufanyika uchaguzi wa amani, wazi na shirikishi.

Burundi Präsident Pierre Nkurunziza
Picha: Getty Images/AFP/F.Guillot

Chama Tawala nchini humo cha CNDD/FDD kimesema uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa utafanyika jumatatu ijayo kama ilivyopangwa,licha ya miito ya kimataifa kutaka zoezi hilo liahirishwe kufuatia wiki kadhaa za machafuko.

Afisa wa chama hicho ambacho wiki hii kimesusia mkutano na upinzani ulioitishwa na umoja wa mataifa, amesema mkutano huo ulilenga kuvuruga uchaguzi. Chama cha CNDD/FDD kimekabiliwa na mapasuko baada ya mwanachama wake wa cheo cha juu ambaye pia alikuwa makamu wa pili wa rais Gervais Rufyikiri kukimbia nchi hiyo, akidai alipokea vitisho kwa sababu ya msimamo wake wa kutounga mkono awamu nyingine ya urais kwa Nkurunziza.

Wakati huo huo, karibu wanafunzi 100 wa chuo kikuu nchini Burundi wametafuta hifadhi katika ofisi ya ubalozi wa Marekani kutokana na hofu ya kisiasa ya nchi hiyo,ubalozi huo ulithibitisha.

Wanafunzi waliweka kambi katika eneo linalofanyiwa ujenzi karibu na viwanja vya ubalozi baada ya chuo chao kufungwa mnamo tarehe 3o Mwezi Aprili kutokana kwa mgogoro huo wa kisiasa.

Polisi iliwaamrisha wanafunzi hao kuondoka katika eneo hilo na baadhi yao walikwenda kwenye eneo la maegesho la ubalozi, ilisema taarifa hiyo, na kuongeza kuwa wanne kati yao walipata majeraha madogo madogo wakati wa tukio hilo.

Mwandishi:Salma Mkalibala/APE/AFPE/REUTERS

Mhariri:Iddi Ssessanga