Vyama vya siasa Tanzania vyaanza kunadi sera zao
31 Agosti 2020Vyama vya siasa nchini Tanzania vimeanza wiki nyingine muhimu ya kuzungumza na wananchi baada ya baadhi yao kuzindua kampeni zao mwishoni mwa wiki. Wakati hali ikiwa hivyo, chama cha ACT Wazalendo kinazindua ilani yake leo Jumatatu tayari kwa kuanza kujinadi kwa wananchi.
Jumla ya wagombea 15 wamejitosa kwenye kinyang'anyiro hicho, lakini hata mmoja wao mwenye uhakika wa kujua na kupima nanma anavyokubalika mbele ya wapigakura wanaofikia milioni 29.
Suala la kura za maoni safari linaonekana kutupwa kapuni na hakuna taasisi wala shirika lolote iliyojitokeza kufanya hivyo, na huenda hali hiyo imechangiwa na sheria kali zinazohusu utafiti na takwimu.
Soma pia: NEC yasema maandalizi ya uchaguzi Tanzania yanaendelea vyema
Ni nini kikwazo dhidi ya kura za maoni?
Wale wanaotaka kuendesha utafiti wowote wanapaswa kwanza kupata kibali kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi Costech na kisha kabla ya utafiti huo kutolewa hadharani unapaswa pia kuridhiwa na tume hiyo.
Hata hivyo, wakati ambapo uchaguzi na mwelekeo wa kisiasa wakati mwingine huendeshwa kisayansi hivyo kukosekana kwa kura za maoni ingawa hakuwezi kuathiri mwelekeo wa uchaguzi wenyewe, lakini ni moja ya karata muhimu inayoweza kutumiwa na wagombea kupangilia vipaumbele vyao.
Soma pia: Tume ya uchaguzi Tanzania yataja majina manne ya wagombea urais
Mtaalamu wa masuala ya siasa na utawala aliyeko nchini Marekani, taifa ambalo nalo pia linajiandaa na uchaguzi mkuu mwezi Novemba, Profesa Boaz amesema kuwa mara nyingi kura za maoni hutumika kama turufu inayoweza kubadilisha upepo wa kisiasa kwa wagombea wengi.
Umuhimu wa kura za maoni katika uchaguzi ni upi?
Mara ya mwisho Tanzania kuendesha kura za maoni kuhusiana na uchaguzi mkuu ilikuwa mwaka 2015, kulikofanyika tafiti mbili ambazo zilitoa matokeo yaliyokaribiana kwa kiasi fulani. Utafiti wa kwanza ulimpa alama kubwa mgombea wa CCM wakati ule mwingine ulisema mgombea aliyekuwa akiungwa mkono na umoja wa ukawa, alikuwa ananafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye uchaguzi huo.
Soma pia: Je demokrasia ya Tanzania inakua au imedumaa?
Lakini mwaka huu jambo hilo halijafanyika tena. Mwandishi wa habari wa siku nyingi na mchambuzi wa mambo, Pascally Mayala anaona kwamba huenda ushawishi unaoletwa na kura za maoni ndiyo moja ya sababu ya jambo hilo kuwekewa kizingiti nchini.
Katika uchaguzi wa mwaka huu ingawa kumekuwa na wagombea 15, hata hivyo ushindani mkali unatarajiwa kujitokeza kwa vyama vitatu, chama tawala CCM, chama kikuu cha upinzani Chadema na chama kilichopata uungwaji mkono kutoka kwa makundi mengi ya watu ACT Wazalendo.