1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Vyama tawala vyapata muafaka kuhusu wahamiaji

Daniel Gakuba
6 Julai 2018

Vyama 3 vinavyounda serikali ya Ujerumani vimepata muafaka kuhusu namna ya kuwashughulikia wakimbizi wanaoingia Ujerumani baada ya kusajiliwa katika nchi nyingine. Muafaka huo unaepusha kuvunjika kwa serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/30vQq
Grenzkontrolle in Bayern
Picha: Getty Images/C.Stache

Muafaka huo uliopatikana baada ya majadiliano mafupi yaliyofanyika kati ya vyama vyote vitatu katika serikali ya mseto inayoongozwa na Kansela Angela Merkel, umehitimisha kipindi cha msukosuko uliotishia kuiangusha serikali ya Kansela Angela Merkel, miezi michache baada ya kuundwa kupitia mchakato mgumu. Mzozo ulidhihirika baada ya waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Christian Social Union, CSU cha jimboni Bavaria, kutishia kukaidi maagizo ya Kansela Merkel, na kuwatimua mpakani waomba hifadhi ambao wamesajiliwa katika nchi nyingine.

Vyama vitatu vinavyounda serikali, Christian Democratic Union, CDU cha Kansela Angela Merkel, CSU cha Horst Seehofer pamoja na chama cha Social Democrats, SPD, vimekubalianakuharakisha shughuli ya kuwarejesha waomba hifadhi katika mataifa walikosajiliwa kwanza, kulingana na sheria za sasa za Umoja wa Ulaya, lakini ikiwa tu yatafikiwa makubaliano kati ya Ujerumani na nchi husika.

Haja ya makubaliano na nchi nyingine

Ili hatua hizo ziweze kutekelezwa kikamilifu, Ujerumani italazimika kufikia kwanza makubaliano na nchi kama Italia na nyingine kadhaa, ambazo zimekuwa zikipinga kuwapokea tena wahamiaji hao wasiotakiwa Ujerumani.

Deutschland Asylstreit Koalitionsausschuss Nahles
Andrea Nahles, Mwenyekiti wa chama cha SPDPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Chama cha SPD kimeyasifu makubaliano hayo kikisema ni ushindi kwake. Mkuu wa chama hicho Andrea Nahles amefurahia kuondolewa kwa wazo la vituo vya wakimbizi vya mpakani, vilivyokuwa vimependekezwa na vyama vya kihafidhina.

''Hakutakuwepo hatua za upande mmoja  juu ya kuwazuia wakimbizi mpakani, badala yake, mchakato wa kushughulikia maombi ya wanaotafuta hifadhi utaharakishwa. Hakuna marekebisho yanayohitajika kuhusu hili, kwa sababu yanaheshimu sheria iliyopo. Hakutakuwepo aina yoyote ya kambi, ambazo kimsingi SPD imezikataa tangu mwanzo.'' Amesema Bi Nahles.

Kutokana na shinikizo la Seehofer na chama chake cha CSU, chama cha CDU cha Kansela Merkel kilikuwa kimeridhia mapema wiki hii, mpango wa kujenga kambi za wahamiaji mpakani, wazo ambalo SPD ililipinga na kutishia kujiondoa katika serikali ya mseto iwapo lingetekelezwa.

CSU pia chaamini kimeshinda

Deutschland Asylstreit Koalitionsausschuss Seehofer
Horst Seehofer, msimamo wake mkali kuhusu wahamiaji umeifikisha serikali ya Ujerumani kwenye ukingo wa kuvunjikaPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Lakini chama cha CSU kinaamini pia kwamba kimeibuka mshindi katika majadiliano ya jana. Mkuu wake, Horst Seehofer alisema matakwa yao yote yamekubaliwa, akidai kilichobadilishwa ni jina tu.

Amesema, ''Utakuwepo mchakato wa mpito na vituo vya polisi, vitu ambavyo tumekuwa tukivitaka. Mnajua, muungano haukupendezwa na jina ''kambi za mpito'', na kwa hivyo, tumetumia ''mchakato wa mpito kwenye vituo vya polisi'' na hivyo ndivyo tutakavyofanya kazi mpakani. Kwetu hilo ndilo muhimu.''

Ingawa makubaliano haya mapya yameepusha kuvunjika kwa serikali ya Kansela Merkel, mvutano huo kuhusu sera ya wahamiaji umedhihirisha udhaifu wa serikali ya sasa ya Ujerumani, na unaacha uwezekano wa kuibuka mizozo mingine siku za usoni.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre,afpe, dw
Mhariri: Iddi Ssessanga