Vyama vidogovidogo Tanzania kuzindua kampeni
4 Septemba 2020Baadhi ya vyama vinaonekana kukabiliwa na ukosefu wa fedha hali ambayo kampeni zao zimekuwa za kusuasua. Licha ya kuwepo wagombea 15, lakini ni wagombea watatu tu wa CCM, Chadema na ACT Wazalendo wanaoonekana kuendelea kupamba majukwaa ya kampeni.
Vyama hivyo ambavyo havikubahatika kuambulia chochote katika uchaguzi uliopita wa 2015, vinajitupa tena kwenye kinyang'anyiro hiki, inasemekana vingine vitaanza kushuka kwenye majukuwaa kuanzia Jumamosi ikiwa zimepita sasa wiki mbili tangu dirisha hilo la kampeni lifunguliwe hapo Agosti 26.
Wagombea hao wa urais wamegawika kwa sera, ikiwamo wale wanaojinadi kwa kauli mbiu ya Tanzania yenye furaha inawezekana,wakimaanisha kuwarejeshea wananchi maisha ya furaha kwa kuwapunguzia ugumu wa maisha na kuwaharakishia maendeleo.
Wengine wanapita mitaani kwa madai ya kuwasogezea karibu huduma zitakazohusu maisha yao kama vile kuwasambazia chakula ikiwamo ubwabwa. Na kwa mara ya kwanza chama cha wanachi Cuf ambacho katika chaguzi zote kiliweka alama kubwa kutokana na ushawishi wake, safari hii kimejikuta kikitumbukia katika kapu moja na baadhi ya vyama vingine ambavyo kampeni zake zinafanyika kimya kimya.
Wagombea wa urais wa vyama kama CCM,Chadema na ACT Wazalendo ndiyo wanaotawala zaidi majukuwaa ya kampeni na wagombea wao mbali na kumwaga sera zao lakini pia wameendelea kutupiana vijembe, kwa kuonyeshana ukosoaji wa waziwazi.
Mgombea wa chama tawala CCM, Rais John Magufuli aliyeko katika eneo la kanda ya ziwa anasema akipewa kipindi kingine cha miaka mitano, yale aliyoyafanya awamu ya kwanza atayaongeza maradufu.
Hoja ya kuwajali wakulima kwa kuwatafutia bei nzuri, kupunguza msuururu wa kodi pamoja na kupitia upya sera ya elimu ni baadhi ya mambo ambayo mgombea wa chadema, Tundu Lissu ambaye leo anawasili mkoani Mbeya ni baadhi ya mambo ambayo amehaidi kuyapa kipaumbele iwapo atachaguliwa Oktoba 28.
Mgombea wa ACT Wazalendo, Bernard Membe ambaye amewahi kuwa serikali ya CCM katika utawala uliopita amekuwa akionyesha ukosoaji wake wa waziwazi kwa utawala wa sasa na kusisitiza kuwa kama atapewa ridhaa ya kuingia ikulu, atawarejeshea matumaini wananchi.
Wagombea hao wanaendelea kwenye kampeni lakini hakuna ishara yoyote kama wanaweza kukutana jukwaa moja kwa mdahalo wa wazi kabla ya kuingia siku ya uchaguzi.