1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu zatokea Uganda baada ya kukamatwa Bobi Wine

18 Novemba 2020

Ghasia zimezuka katika miji mbalimbali ya Uganda kufuatia kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi.

https://p.dw.com/p/3lVeZ
Uganda Kampala Proteste nach Festnahme von Bobi Wine
Picha: Reuters/Stringer

Picha za angalau watu watatu wanaoaminika kuuawa katika ghasia hizo mjini Kampala pekee zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii huku mwanasiasa huyo akiendelea kushikiliwa katika korokoro ya polisi mjini Jinja ambayo imezingirwa na majeshi na polisi.

Milio ya risasi na mabomu ya gesi ya kutoa machozi ndiyo imehanikiza alasiri ya leo mjini Kampala wakati polisi walipokabiliana na waandamanaji wakidai kuachiwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi. 

Uganda Kampala Proteste nach Festnahme von Bobi Wine
Picha: Reuters/Stringer

Shughuli zimesimama katika mji wa Kampala wakati waandamanaji walipowasha moto katikati mwa barabara na katika ghasia hizo watu kadhaa wamejeruhiwa. Taarifa ambazo hazijathibitishwa rasmi zinasema kuwa angalau watu watatu wameuawa. 

Kumeshuhudiwa michirizi ya damu iliyotapakaa kwenye barabara kuu ya Kampala.

Ghasia zimeripotiwa kutokea katika miji mingine ikiwemo Jinja ambako mwanasiasa Bobi Wine anaelezwa kuzuiliwa katika korokoro ya Nalufenya.

Kanuni za COVID-19 ndiyo chanzo 

Kukamatwa kwa Bobi Wine kunatokea siku moja tu baada ya mkuu wa jeshi la polisi kuwaonya makamanda wa jeshi hilo kuwa watawajibika na kuadhibiwa ikiwa wataruhusu wagombea kukiuka kanuni za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.

Bildergalerie Persönlichkeiten 2020 | Bobi Wine
Picha: Getty Images/L. Dray

Hata hivyo, wanasiasa wa upinzani wanasisitiza kuwa kanuni za kudhibiti COVID-19 zinatumiwa tu kama kisingizio cha kuwakandamiza.

Hata hivyo kuna baadhi ya wanasiasa wa upinzani ambao wanawakosoa wenzao kwa kukaidi mwongozo waliopewa katika kuendesha kampeni hizo.

Kulingana na kanuni hizo mgombea haruhurusiwi kuwa na mkutano wa zaidi ya watu 200 na wote lazima wavalie barakoa.

Hadi wakati wa kutuma wa kuandaa taarifa hii polisi na wanajeshi walikuwa wameshika doria kali katikati ya mji na watu wengi wameshuhudiwa wakitafuta namna ya kurudi makwao.