1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuguvugu la Mrengo wa kushoto magazetini

Oumilkheir Hamidou
5 Septemba 2018

Vuguvugu linaloyaleta pamoja makundi na vyama vya mrengo wa kushoto,"Aufstehen" au "Amkeni", mpango wa mageuzi katika jeshi la shirikisho na pambano jipya la dimba barani Ulaya-Nations League ndizo mada magazetini

https://p.dw.com/p/34KR1
Deutschland | PK Vorstellung der linksgerichteten Sammelbewegung #Aufstehen
Picha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrcenka

Tunaanzia Berlin ambako jana mkuu wa kundi la wabunge wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke, Sahra Wagenknecht alizinduwa rasmi "vuguvugu jipya la mrengo wa kushoto kwa jina "Aufstehen" au Amkeni. Vuguvugu hilo lililoanzishwa mtandaoni limeshajikusanyia zaidi ya wafuasi laki moja. Na uchunguzi wa maoni unaonyesha wajerumani wengi zaidi wanavutiwa na lengo la vuguvugu hilo. Hata hivyo gazeti la mjini Dresden "Sächsische Zeitung" linahisi vuguvugu hilo lina ila. Gazeti linaendelea kuandika:"Mrengo wa kushoto unaovutia na unaoaminika unaweza kuwa na faida kubwa kwa nchi. Lakini vuguvugu la Aufstehen halitamudu hayo.Tatizo lake linaanzia kwa waanzilishi wa vuguvugu hilo: Oskar Lafontaine na Sahra Wagenknecht wana uwezo wa kufanya mengi lakini  sio wa kuwaleta watu pamoja seuze kuwaunganisha. Na mwishoe wafuasi wa vuguvugu la "Aufstehen" watabidi wamchague yupi kati ya hao wawili?"

 Ila zinatajwa pia na gazeti la mjini Koblenz "Rhein Zeitung" linaloandika:

"Vuguvugu la "Aufstehen" lina hoja nzito na za haki: Wanataka kuhakikisha mitaa ya Ujerumani haidhibitiwi na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wanaotaka kuzigeuza kero za wajerumani kuwa maandamano ya chuki dhidi ya wageni kuanzia Chemnitz na kuzieneza katika sehemu nyengine za Ujerumani. Lakini kama tija ya vuguvugu hilo itakuwa mmomonyoko wa vyama  zaidi vya kidemokrasi, basi Wagenknecht na wenzake watakuwa hawajasaidia kuimarisha si utulivu na wala si usalama. Kwamba mpaka kiongozi wa AfD Alexander Gauland anasifu "kuzinduliwa vuguvugu la Aufstehen" hilo linabidi liwazinduwe waasissi wa vuguvugu hilo."

Jeshi la shirikisho lahitaji mageuzi

Ripoti kuhusu umuhimu wa kufanyiwa marekebisho jeshi la shirikisho zimekuwa zikitolewa kila kukicha. Hatimae waziri wa ulinzi bibi Ursula von der Leyen amechapisha mpango kabambe wa jinsi ya kuliambatanisha na wakati jeshi hilo. Gazeti la "Neue Westfälische linaandika: "Ursula von der Leyen ametambua wakati namna ulivyo. Na ameamua. Kwa miaka jeshi la shirikisho Bundeswehr lilikuwa likilinganishwa na mama wa kambo. Hivi sasa mipango imeshaandaliwa ya kuligeuza jeshi la Ujerumani liwe la kimambo leo. Pesa zitatengwa kwaajili ya vikosi vya wanajeshi. Hadi mwaka 2023 matumizi ya kila mwaka ya jeshi la shirikisho yatafikia Euro bilioni 60. Bila ya shaka enzi za vita baridi na miradi ya kujirundikia silaha zimeshamalizika. Lakini Bundeswehr linakabiliwa na changamoto za aina mpya na linabidi liwajibike. Juhudi zake kimataifa zinazidi kuongezeka  kwa hivyo wanajeshi na vifaa pia wanabidi wazidishwe.

 Faida ya pambano jipya la Nations League

Mada ya mwisho magazetini inatuteremsha viwanjani. Pambano jipya la dimba linaaanza kesho kati ya mabingwa wa dunia Ufaransa na timu ya taifa ya Ujerumani iliyopata pigo kubwa kwa kupigwa kumbo katika duru za mwanzo mwanzo za kombe la dunia msimu wa kiangazi uliopita nchini Urusi.Gazeti la "Volksstimme" linazungumzia kuhusu pambano hilo jipya na umuhimu wake."Linaitwa vipi" Viongozi wa dimba wamebuni pambano jipya. Mbali na kombe la dunia la dimba na kinyang'anyiro cha kuania ubingwa barani Ulaya, timu za taifa barani Ulaya siku za mbele zitakuwa na kinyang'anyiro cha "Ligi ya mataifa",au "Nations League".

Eti hiyo ni njia ziada ya kujikusanyia mapato?  Na wanasoka  jee, si wanazidishiwa mzigo wa kazi hivyo.? Bila ya shaka watu hawana maoni sawa linapohusika suala kama pambano hilo lina maana yoyote au la. Na nani ataibuka na ushindi pambano litakapomalizika, nalo pia si suala muhimu sana. Muhimu zaidi ni ule ukweli kwamba Ujerumani inapata fursa ya kupimana nguvu na Ufaransa baada ya pigo la kombe la dunia."

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman