Vuguvugu la MK la Uganda lajigeuza asasi ya kiraia
8 Februari 2024Vuguvugu la MK, ambalo miezi 17 iliyopita lilizinduliwa kama chombo cha kumpigia debe jenerali Muhoozi Kainerugaba kumrithi baba yake, sasa limejitangaza kuwa Shirikisho la Uzalendo la Uganda (PLU), ambapo viongozi wake wamejielezea kuwa wao ni kundi la kuhamasisha uzalendo, mshikamano na maendeleo wakishtumu vikali mienendo ya ufisadi.
"Sisi wanavuguvugu la MK tunatangaza malengo ya umoja na mshikamano kuwa kielelezo chetu cha kuwa asasi ya kiraia itakayojulikana kama Patriotic League of Uganda." Alisema mratibu wa kundi hilo, Michael Mawanda, wakati wa uzinduzi wa PLU.
Soma zaidi: Mtoto wa Museveni azusha mjadala kwa kuiunga mkono Urusi
Hatua hiyo ya wafuasi na mashabiki wa Jenerali Muhoozi kujitangaza kubadili jina lao kutoka MK Movement na kuwa Patriotic League of Uganda inatazamwa na wengine kuwa njia ya kumkinga na kumwezesha kushiriki siasa bila kuhitilafiana na sheria kwamba afisa wa jeshi asishiriki masuala ya siasa.
Wanaelezea kuwa yote yanayofanyika yanadhihirisha kuwa Muhoozi ana kiu ya kutawala Uganda akimrithi baba yake, ambaye baadhi ya wanasiasa ndani ya chama wanaukosowa utawala wake kwa kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
"Hata sisi katika chama tawala cha NRM tumepiga kelele kushutumu mapungufu kama ufisadi lakini sasa tunatarajia suluhu katika PLU," alisema Margaret Muhanga, ambaye ni waziri wa nchi katika wizara ya afya.
Njia ya Muhoozi kuelekea Ikulu?
Lakini baadhi ya watu wana maoni kuwa hii ndiyo itakayokuwa njia ya kupokezana madaraka kwa amani nchini Uganda wakimwandaa Muhoozi kujenga misingi ya uzalendo na uongozi wake kueleweka zaidi na wananchi.
Mmoja wao ni Mike Mukula, ambaye miongoni mwa viongozi wakuu wa chama tawala cha NRM na ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa afya. Mukula alisema kwamba "Yoweri Kaguta Museveni ametimiza jukumu lake sasa ni nyie vijana kuiendeleza Uganda kama ilivyofanyika kule Cuba, Korea kaskazini, Afrika Kusini na hata Tanzania."
Soma zaidi: HRW: Uganda ichunguze ukandamizaji wa wanaharakati
Uwezekano wa PLU kutumika kama jukwaa la kisiasa nje ya mfumo wa chama tawala cha NRM ni mkubwa, kwani Mawanda alisema kuwa wanatazamia "kuwa na mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026."
Jenerali Muhoozi mwenyewe hakuwepo katika uzinduzi huo wa PLU, ambao ulihudhuriwa na wabunge zaidi ya 50 wakiwemo wawili kutoka chama kikuu cha upinzani NUP kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.
Mwaka 2023, Jenerali Muhoozi alijitangaza kwamba angegombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026 huku akisambaza taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii ambazo ziliwaghadhabisha baadhi ya watu hata katika nchi jirani ya Kenya.
Ilibidi baba yake kuingilia kati akimwonya kuacha kujihusisha moja kwa moja katika masuala ya kisiasa.