1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen: Mianya mikubwa ingalipo kuhusu Brexit

18 Desemba 2020

Boris Johnson na Ursula von der Leyen, wasema licha ya muelekeo kwenye mazungumzo ya biashara ya baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, lakini bado kuna mianya kadhaa ambayo inatatiza ufumbuzi. 

https://p.dw.com/p/3mtvt
Belgien EU Brexit l EU-Kommissionspräsidentin von der Leyen und der Britische Premierminister Johnson
Picha: Olivier Hoslet/AP/picture alliance

Viongozi wa Uingereza pamoja na wenzao wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, hawakuwa na matumaini makubwa kwenye mazungumzo ya kibiashara ya baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo, ambayo yanaweza kuiepusha Uingereza kujiondoa katika Umoja huo bila ya makubaliano.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameonya kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kukosekana makubaliano, hali ambayo itailazimu Uingereza kujitoa bila ya mkataba.

Utata kuhusu haki ya uvuvi

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema hatua kubwa zimepigwa kuhusu masuala kadhaa, lakini suala kuhusu haki ya uvuvi limesalia kuwa tete.

Von der Leyen amesema wamekaribisha hatua kubwa ambazo zimepigwa kuhusu masuala mengi. Lakini bado kuna mianya mikubwa inayopaswa kuzibwa hususan kuhusu suala la uvuvi, hali ambayo itakuwa changamoto kubwa kuziba. Amesema hayo baada ya mazungumzo ya Alhamisi usiku na kuongeza kwamba mazungumzo zaidi yataendelea Ijumaa.

Yapo masuala matatu ambayo ni tete, lakini utata zaidi ni swali kuhusu mipaka ya baharini kwa Umoja wa Ulaya kuvua samaki katika maeneo ya bahari ndani ya Uingereza.

Muda wayoyoma kwa pande zote kuafikiana

Zikiwa zimesalia siku chache tu kufikia Disemba 31, ambayo ndiyo tarehe iliyowekwa kwa pande zote kuafikiana, Uingereza imeonekana kuchukua msimamo legevu wa kupoteza matumaini ya kupatikana makubaliano.

Boris Johnson amerudia kusema kwamba muda uliosalia ni mfupi. Hayo ni kulingana na msemaji wake aliyeongeza kuwa ikiwa hawatakubaliana, basi Uingereza na Umoja wa Ulaya zitatengana kama marafiki, ambapo zitafanya biashara kwa kufuata mfumo wa Australia. Ifahamike kuwa Australia haina mkataba wowote wa biashara huru na Umoja wa Ulaya.

Uingereza ilijitenga rasmi na Umoja wa Ulaya Januari 31, 2020 lakini masuala kuhusu biashara na sekta nyingine yameendelea kuwa chini ya Umoja wa Ulaya hadi mwisho wa mwaka huu.

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Olivier Hoslet/REUTERS

Nini itafanyika makubaliano yakikosekana?

Ikiwa Disemba 31 itapita bila ya makubaliano, basi biashara kati ya pande zote mbili itafuata sheria na kanuni za ushuru zilizotungwa mwaka 1995 na Shirika la Biashara Duniani WTO. Pande zote zitahitajika kulipa ushuru kwa bidhaa zitakazoagiza.

Wajumbe wa mashauriano hayo wameshiriki vikao vingi vya mazungumzo bila ya kuafikiana kuhusu masharti ya kibiashara.

Mazungumzo hayo yamekuwa yakifeli pakubwa pia kwa sababu ya Uingereza kusisitiza kwamba inapaswa kufanya biashara na Umoja wa Ulaya kwa masharti machache, lakini Umoja wa Ulaya inashikilia kuwa Uingereza lazima ifuate sheria zake ili kuwe na ushindani wenye usawa.

Uingereza inadai kuwa Umoja wa Ulaya inakusudia kukiuka hadhi ya Uingereza kama taifa huru  yenye mamlaka yake, kwa kuilazimisha kuheshimu sheria za umoja huo.

Kwa upande mwingine, Umoja wa Ulaya unahofia kwamba Uingereza inaweza kushusha pakubwa viwango vyake vya kijamii na kimazingira, huku ikitoa fedha za serikali kupiga jeki sekta yake ya viwanda, hivyo kuwa na mpinzani kwenye viwango vya chini vya ukaguzi wa uchumi pembezoni mwake

/dw/en/brexit-some-progress-more-gaps-as-uk-eu-race-to-lock-down-trade-deal/a-55981170