Von der Leyen: kutoka Berlin mpaka Brüssel?
3 Julai 2019Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen , bila kutarajiwa ametarajiwa kuchukua wadhifa wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya. Von der Leyen ni kiongozi mwenye vipaji vingi. Ni nani basi Ursula von der Leyen , huu hapa wasifu wake kama ulivyoandikwa na Christioph Strack , na kusomwa sutudioni na Sekione Kitojo.
Miaka 60 iliyopita alizaliwa katika mji wa Brussels. Na sasa inawezekana kuwa njia yake ya kisiasa ghafla inamuelekeza tena katika mji huo mkuu wa Ubelgiji na mji mkuu wa Umoja wa Ulaya. Jana Jumanne viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kwa pamoja kwamba Ursula von der Leyen atakuwa kiongozi wa Umoja huo.
Maisha ya Ursula von der Leyen
Katika miaka yake 13 ya mwanzo ya maisha yake von der Leyen alikuwa mjini Brussels. Baba yake, ambaye baadaye alikuja kuwa waziri mkuu wa Uholanzi Ernst Albrecht, alifanyakazi wakati huo katika wadhifa wa uongozi katika taasisi ya Jumuiya ya Umoja wa nchi za Ulaya, taasisi ambayo ilikuwa kabla ya Umoja wa Ulaya.
Von der Leyen anazungumza kiingereza na Kifaransa kwa fasaha kuliko baadhi ya wenzake katika baraza la mawaziri, na ni mtu anayeonekana wakati wote kuwa wa kimataifa. Katika baraza la mawaziri la kansela Merkel von der Leyen amekwisha shika nyadhifa mbali mbali.
Umakini wa utendaji kazi wake
Na kila mara huchukulia kwa dhati wadhifa mpya anaopewa , huuliza maswali , hujaribu kubadilisha taratibu na kuangalia kwa makini kuyatumia madaraka aliyopewa na pia kuchukua tahadhari katika ushirikiano na vyama vinavyounda serikali.
Ni mama wa watoto saba na alikuwa waziri wa masuala ya famiali tangu mwaka 2005 hadi 2009 na alifanikiwa kwa sehemu fulani kuweka ishara kwa utendaji wake.
Alifanikiwa kuanzisha kile kinachofahamika kama fedha kwa ajili ya wazazi pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya mahitaji ya wananchi katika ujenzi nchi nzima wa vituo vya kuwatunza watoto. Mwaka 2009 katika wadhifa wa pili katika baraza la mawaziri la kansela Merkel, von der Leyen ambaye amesomea udaktari aliteuliwa kuwa waziri wa afya.
Miaka minne baadaye , mwezi Desemba 2013 , alibadilishwa kuwa waziri wa ulinzi, wadhifa huu ameushikilia hata baada ya mabadiliko ya serikali baada ya uchaguzi wa mwaka 2017 ambapo serikali iliundwa pamoja na chama cha SPD.
Waziri huyo mwanamke baada ya kupata mbinyo mkubwa kutoka kwa wafanyakazi na hata vyombo vya habari kutaka kuongeza idadi ya wanajeshi. Alibadili hali hiyo kwa kauli mbiu ya "mabadiliko ya wafanyakazi", waziri Von der Leyen alifanikiwa kuzuwia kunywea kwa idadi ya wanajeshi katika jeshi la Ujerumani na hatimaye kufikisha idadi ya wanajeshi 185, 000.
Lakini hata hivyo aliyumba kidogo von der Leyen, licha ya kuonekana kama mtendaji katika miaka iliyopita. Kuna mambo yaliyomchafua binafsi , lakini pia kutokana na kashfa mbali mbali. Katika wakati wake wa uongozi kulikuwa na matatizo makubwa ya mradi wa ununuzi wa silaha. Kulikuwa pia na wafanyakazi wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia katika jeshi, na bila shaka kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake alijiweka kando na vikosi vya jeshi.