1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen: kutoka Berlin mpaka Brüssel?

Sekione Kitojo
3 Julai 2019

Waziri wa  ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen , bila  kutarajiwa ametarajiwa kuchukua  wadhifa  wa  rais  wa  halmashauri  ya  Umoja wa  Ulaya. Von der Leyen  ni  kiongozi mwenye vipaji  vingi.

https://p.dw.com/p/3LUzb
Ursula von der Leyen Verteidigungsministerin
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen , bila  kutarajiwa ametarajiwa kuchukua  wadhifa  wa  rais  wa  halmashauri  ya  Umoja wa  Ulaya. Von der Leyen  ni  kiongozi mwenye vipaji  vingi. Ni  nani basi  Ursula von der Leyen , huu hapa wasifu  wake kama ulivyoandikwa na Christioph Strack , na  kusomwa  sutudioni  na  Sekione Kitojo.

Miaka 60 iliyopita  alizaliwa  katika  mji  wa  Brussels. Na  sasa inawezekana  kuwa  njia yake  ya  kisiasa  ghafla  inamuelekeza  tena katika  mji  huo  mkuu  wa  Ubelgiji na mji  mkuu wa  Umoja  wa  Ulaya. Jana  Jumanne  viongozi  wa  Umoja  wa  Ulaya  walikubaliana  kwa pamoja  kwamba  Ursula von der Leyen atakuwa  kiongozi  wa  Umoja huo.

Maisha ya  Ursula von der Leyen

Schwielowsee  Ursula von der Leyen Bundeswehr Foreign Operations Command
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der LeyenPicha: Getty Images/S Gallup

Katika miaka  yake 13  ya  mwanzo ya maisha  yake  von der Leyen alikuwa  mjini  Brussels. Baba  yake, ambaye  baadaye  alikuja  kuwa waziri  mkuu  wa  Uholanzi  Ernst Albrecht, alifanyakazi  wakati  huo katika  wadhifa  wa  uongozi  katika  taasisi  ya  Jumuiya ya  Umoja  wa nchi za Ulaya, taasisi ambayo  ilikuwa  kabla  ya  Umoja  wa  Ulaya.

Von der Leyen  anazungumza kiingereza  na  Kifaransa kwa  fasaha kuliko  baadhi  ya  wenzake katika  baraza  la  mawaziri, na  ni  mtu anayeonekana  wakati  wote  kuwa  wa  kimataifa. Katika  baraza  la mawaziri  la   kansela  Merkel  von der Leyen  amekwisha  shika nyadhifa  mbali  mbali.

Umakini wa utendaji kazi wake 

Na kila  mara  huchukulia  kwa  dhati  wadhifa  mpya  anaopewa , huuliza  maswali , hujaribu  kubadilisha  taratibu na kuangalia  kwa makini  kuyatumia  madaraka  aliyopewa  na  pia kuchukua  tahadhari katika ushirikiano  na  vyama  vinavyounda  serikali.

Ni mama wa watoto saba na alikuwa waziri wa masuala ya famiali tangu mwaka 2005  hadi 2009 na  alifanikiwa  kwa  sehemu  fulani kuweka  ishara kwa  utendaji  wake.

Alifanikiwa kuanzisha  kile  kinachofahamika  kama  fedha  kwa  ajili  ya wazazi pamoja na kutenga  fedha  kwa  ajili  ya  mahitaji ya  wananchi katika ujenzi  nchi  nzima wa  vituo  vya  kuwatunza  watoto. Mwaka 2009  katika  wadhifa  wa  pili  katika  baraza  la  mawaziri  la  kansela Merkel, von der Leyen  ambaye  amesomea  udaktari  aliteuliwa  kuwa waziri  wa  afya.

Miaka  minne  baadaye , mwezi  Desemba  2013 , alibadilishwa  kuwa waziri  wa  ulinzi, wadhifa  huu  ameushikilia  hata  baada  ya  mabadiliko ya  serikali  baada  ya  uchaguzi  wa  mwaka  2017 ambapo serikali iliundwa  pamoja  na  chama  cha  SPD.

Waziri  huyo  mwanamke baada ya kupata  mbinyo mkubwa  kutoka kwa wafanyakazi  na  hata  vyombo  vya  habari kutaka  kuongeza  idadi ya  wanajeshi. Alibadili  hali  hiyo kwa  kauli mbiu ya "mabadiliko ya wafanyakazi", waziri  Von der Leyen  alifanikiwa  kuzuwia  kunywea  kwa idadi  ya  wanajeshi katika  jeshi  la  Ujerumani  na  hatimaye  kufikisha idadi  ya  wanajeshi 185, 000.

Lakini  hata  hivyo aliyumba  kidogo von der Leyen, licha  ya kuonekana  kama mtendaji katika  miaka  iliyopita. Kuna mambo yaliyomchafua  binafsi , lakini  pia  kutokana na  kashfa  mbali  mbali. Katika  wakati  wake  wa  uongozi  kulikuwa  na  matatizo  makubwa ya mradi wa ununuzi  wa silaha. Kulikuwa  pia  na  wafanyakazi wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia katika  jeshi, na bila shaka kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake alijiweka kando na vikosi vya jeshi.