1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen afanya ziara nchini Marekani

Angela Mdungu
10 Machi 2023

Raisi wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula Von der Leyen yuko ziarani nchini Marekani ambako atakutana Ikulu baadaye leo na Rais Joe Biden. Wawili hao watazungumza na vyombo vya habari baada ya mazungumzo yao.

https://p.dw.com/p/4OWcZ
Frankreich | Europäisches Parlament - Sitzung zum Ukraine-Krieg
Picha: Jean-Francois Badias/AP/dpa/picture alliance

Msemaji wa kamisheni ya Ulaya katika masuala ya biashara na kilimo Miriam Garcia Ferrer ameiambia DW kuwa moja ya madhumuni ya ziara Von Der Leyen ni kuwa Umoja wa Ulaya unataka kuondokana na ubaguzi wa makampuni  na bidhaa za Umoja wa Ulaya kadri wawezavyo na kuepuka upotoshaji katika masuala ya biashara.

Ferrer hakutaka kuthibitibitisha taarifa zozote za matarajio ya kufikiwa kwa makubaliano muhimu. Hata hivyo amesema, Marekani imeonesha nia ya kuwatendea kwa usawa washirika wa biashara huria wa Umoja wa Ulaya na wa Marekani  katika kusambaza madini muhimu linapokuja suala la sheria ya kupunguza mfumuko wa bei.

Maafisa wa  Umoja wa Ulaya  wanawasiwasi kwamba, uwekezaji mkubwa katika uchumi wa kijani nchini Marekani unaweza kuyavutia makampuni ya teknolojia ya Ulaya nchini humo.

Sheria ya kupunguza mfumuko wa bei IRA  imekuwa chanzo cha msuguano katika uhusiano wa kimataifa kwa miezi kadhaa. Awali sheria hiyo ilipongezwa kama hatua ya mabadiliko kwa sera ya hali ya hewa nchini Marekani huku ikitoa mabilioni ya dola kama ruzuku na kuunga mkono teknolojia safi inayotengenezwa kwenye taifa hilo.  Kwa Umoja wa Ulaya, sheria hiyo inaonekana kama inayokwenda kinyume na ushindani, ikisababisha hofu kuwa makampuni ya Umoja huo na watengenezaji wa magari  wanaweza wakashawishika kuwekeza Marekani kwa ahadi ya kusamehewa sehemu kubwa ya kodi.

England | G7 Gipfel 2021 | Joe Biden, Emmanuel Macron und Ursula von der Leyen
Kutoka kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Raisi wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula Von der LeyenPicha: Leon Neal/AP/picture alliance

Ziara ya Von der Leyen si juhudi pekee ya kuyaweka makampuni ya Umoja wa Ulaya katika nafasi nzuri. Kamisheni ya Ulaya inatarajiwa kuweka wazi sheria inayoonekana kuwa jibu la moja kwa moja kwa ruzuku la Marekani ifikapo Jumanne.

Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa na makubaliano ili kupunguza mivutano.

Makubaliano chini ya mjadala huo yanafanywa kwa siri lakini ripoti  zinadai kuwa yanaweza kuwaruhusu wasafirishaji wa bidhaa wa Umoja wa Ulaya kupata fursa ya kupewa ruzuku katika baadhi ya maeneo.  Maeneo hayo ni kama vile vifaa vinavyotumika kuunda betri na madini muhimu.

Mwezi Oktoba, Umoja wa Ulaya na Marekani walianzisha chombo chenye madhumuni ya kuyaainisha mambo yaliyo kwenye mzozo kati ya pande hizo mbili. Ingawa kutokukubaliana kuhusu ruzuku kwa uchumi wa kijani kumeathiri mahusiano ya Ulaya na Marekani,  mataifa hayo yamekuwa yakisisitiza umoja kutokana na jitihada zao za kupata jibu la pamoja katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.