1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyayaharibu maeneo ya turathi ya Syria

Josephat Nyiro Charo30 Desemba 2014

Umoja wa Mataifa umesema maeneo karibu 300 yenye thamani kubwa kwa Syria na historia ya binadamu yameharibiwa au kuporwa katika vita vilivyodumu takriban miaka minne nchini humo ukitumia ushahidi wa picha za satelaiti.

https://p.dw.com/p/1EDCU
Altstadt von Aleppo (vorher und nachher) BILDKOMBO
Mji mkongwe wa Aleppo kabla na baada ya vitaPicha: US Department of State, Humanitarian Information Unit, NextView License (DigitalGlobe)

Kutoka kwa makazi ya kihistoria na masoko ya kale hadi misikiti mashuhuri na makasri ya wahubiri, Syria ni nyumbani kwa turathi zenye thamani zisizo idadi. Lakini tangu kuzuka vita nchini humo mwaka 2011, maeneo ya turathi yameharibiwa kabisa na pande zote husika katika vita hivyo, wafuasi wa serikali, waasi wanaoipinga serikali, wapiganaji wa jihadi na hata wakaazi waliokata tamaa.

Baada ya utafiti mkubwa Umoja wa Mataifa umesema uchambuzi wa picha za satelaiti kutoka mamia kadhaa ya maeneo umefichua kiwango cha uharibifu uliotokea. Kati ya maeneo 290, 24 yameharibiwa, 104 yamevunjwa vibaya, 85 yameharibiwa kidogo na 77 huenda yameharibiwa. Umoja wa Mataifa umesema ripoti hiyo ni ushuhuda wa kutisha kuhusu uharibifu unaoendelea kwa turathi za kitamaduni za Syria na umetoa mwito juhudi za makusudi zifanyike kuzilinda.

Picha za satelaiti zilikusanywa na UNOSAT, taasisi ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu mjini Geneva, Uswisi, zilijumuisha maeneo 18, sita kati yao yaliyoorodheshwa na shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, kama turathi za kimataifa - Mji wa kale wa Aleppo, Bosra, Damascus, Miji iliyokufa ya kaskazini mwa Syria, kasri la Crac des Chevaliers na kidimbiwi cha maji cha Greco-Roman cha Palmyra.

Carlton Citadel Hotel in Aleppo zerstört (Syrien)
Hoteli ya Carlton iliyoharibiwa AleppoPicha: picture-alliance/AP Photo

"Ni huzuni kubwa kwa Syria na kwa ulimwengu mzima kwamba haya yanatokea," amesema mkurugenzi wa taasisi ya UNOSAT, Einar Bjorgo, wakati alipozungumza na shirika la habari la AFP. "Binadamu wanapoteza mamia na maelefu ya miaka ya turathi," akaongeza kusema mkurugenzi huyo.

Aleppo, mji wa kibiashara wa zamani wa Syria ambako makazi yalianza miaka 7,000 iliyopita, umeathirika sana kutokana na mapigano makali kati ya waasi na vikosi vinavyomtii rais wa Syria Bashar al Assad. Picha za satelaiti zinaonyesha msikiti mkubwa wa Aleppo wa karne ya 11 ulishuhudia mnara wake ukiharibiwa na kuwa kifusi kwenye mapigano hayo na hoteli mashuhuri ya Carlton imeharibiwa, ikiacha shimo kubwa.

Hasara isiyo kifani

Kila mara utawala au waasi wangeuteka msikiti huo, wangeweka walenga shabaha katika mnara wake. Cheikhmous Ali wa shirika la ulinzi wa akiolojia Syria, APSA ameliambia shirika la habari la AFP hatimaye mnara wa msikiti huo ulilengwa katika shambulizi la kutokea angani. Ali ameongeza kusema soko la kale mjini Aleppo, soko kubwa la aina yake ulimwenguni, pia limeharibiwa vibaya.

Picha za Umoja wa Mataifa pia zinaonyesha uharibifu kwa Palmyra huku jeshi la Syria likijenga barabara inayopitia eneo la makaburini na kuyaharibu makaburi kadhaa. Ali aidha amesema barabara hiyo inatumiwa na vifaru na hatua ya kufyetua makombora inavuruga uthabiti wa eneo hilo.

Umayyaden-Moschee in Aleppo zerstört (Syrien)
Msikiti wa Umayyaden ulioharibiwa AleppoPicha: J. Al-Halabi/AFP/Getty Images

Katika mji wa Raqa, ngome ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, msikiti wa Uwais al-Qarni wa waislamu wa madhehebu ya Sufi na eneo takatifu la Ammar ibn Yasir, kwa sehemu kubwa umeharibiwa.

Mkoani Homs eneo la Crac des Chevaliers lililokuwa likidhibitiwa na waasi limepoteza haiba yake na paa lake baada ya kushambuliwa kwa mabomu na vikosi vya serikali. Waasi katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Idlib wameyageuza mojawapo ya makao makuu ya falme za kale za Syria, Ebla, kuwa kambi ya mafunzo.

Cheikhmous Ali wa shirika la ulinzi wa akiolojia Syria, APSA amesema kitisho ni kikubwa zaidi nchini Syria kuliko Iraq. "Hapa maeneo yamegeuzwa kuwa kambi za kijeshi na uwanja wa mapigano. Amesema, "Ni janga kubwa na hasara isiyo kifani kwa binadamu."

Mwandishi:Josephat Charo/AFPE

Mhariri:Iddi Sessanga