UN: Vita vya Gaza vimewaathiri mno wanawake na watoto
17 Aprili 2024Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa wanawake hao hujikuta katika mazingira hatarishi kutokana na majukumu yao ya ulinzi, ustawi, lakini pia kutafuta chakula na maji kwa ajili ya familia zao.
Akitoa taarifa kutoka mjini Cairo kwa waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Tess Ingram, mtaalamu wa mawasiliano katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) amesema:
"Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, idadi kubwa ya watoto wamejeruhiwa katikati ya mashambulizi makali na mara nyingi ya kiholela. Maisha yao daima yamebadilika kutokana na ukatili wa vita. Jumla ya watoto waliojeruhiwa katika mzozo huu ni ngumu mno kutathminiwa, lakini takwimu za hivi punde kutoka kwa Wizara ya Afya ya Palestina inakadiria kuwa zaidi ya watoto 12,000 wamejeruhiwa, ambao ni sawa na takriban watoto 70 wanaojeruhiwa kwa siku huko Gaza tangu kuanza kwa mzozo huu.", alisema Ingram.
Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza hii leo kuwa jumla ya watu 33,899 wameuawa na wengine 76,664 wamejeruhiwa huko Gaza.