1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visa vya mateso na watu kutoweka Burundi vyaendelea

Daniel Gakuba
14 Machi 2017

Visa vya watu kuteswa na kutoweka vinavyoripotiwa kutokea nchini Buruni vimeibua wasiwasi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/2Z8ba
Burundi Pierre Nkurunziza
Picha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa limesema linatiwa wasiwasi na ripoti za mateso na kutoweka kwa watu vinavyoripotiwa nchini Burundi, lakini limepuuza miito ya mashirika ya haki za binadamu kutaka nchi hiyo iwekewe vikwazo. Tangazo lililoandaliwa na Ufaransa kuhusu nchi hiyo limepitishwa kwa kauli moja, baada ya upinzani wa Urusi, China na Misri ambazo zinapinga vikwazo dhidi ya Burundi.

Katika tangazo hilo baraza limesema hali kwa ujumla ni ya utulivu nchini Burundi, na kuongeza lakini kuwa idadi kubwa ya watu wanaendelea kuikimbia nchi hiyo.

Wakati huo huo serikali ya Burundi imetangaza ugonjwa wa Malaria kuwa janga la kitaifa, ikisema maradhi hayo yameuwa watu zaidi ya 700 mwaka huu pekee. Waziri wa afya wa nchi hiyo Josiane Nijimbere amesema idadi ya vifo ni ya kutisha, na kuongeza kuwa akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ndio wanaokabiliwa na kitisho kikubwa zaidi.