Viongozi wakuu wa UN wazitembelea Uturuki na Syria.
11 Februari 2023Mkuu wa kitengo cha misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema leo kuwa tetemeko kubwa la ardhi lililopiga kusini mwa Uturuki na kaskazini magharibi mwa Syria ni tukio baya zaidi katika kipindi cha miaka 100 katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika jimbo la Uturuki la Kahramanmaras, Griffiths pia alipongeza hatua na juhudi za Uturuki kwa kushughulikia janga hilo huku akitumai kuwa msaada unaolekezwa Syria utayafikia maeneo yote, ikiwa yanayodhibitiwa na serikali na yale yanayoshikiliwa na upinzani.
Wakati huo huo, Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus amewasili leo katika mji uliokumbwa na tetemeko la ardhi wa Aleppo na kuzitembelea hospitali na sehemu zinazowahifadhi manusura. Hadi sasa vifo kufuatia janga hilo vimepindukia 25,000.