Viongozi wajadili ujenzi mpya wa Ukraine
4 Julai 2022Viongozi wa nchi na mashirika mbalimbali ya dunia wanajadili huko Uswisi namna ya kuisadia Ukraine katika kile kinachoitwa mpango wa Marshall. Mpango huo unalenga kutoa muongozo wa ujenzi mpya wa Ukraine baada ya vita.
Viongozi kutoka nchi kadhaa na mashirika ya kimataifa wanakutana leo na kesho Jumanne katika mji wa Lugano nchini Uswisi kutafuta mpango mpya wa kusaidia kuijenga upya Ukraine katika kile kinachofananishwa na mpango wa Marshall. Juhudi hizo zinalenga kusaidia kuongeza kasi ya kuijenga upya Ukraine na huenda ukagharimu mabilioni ya dola.
Rais wa Uswisi Ignazio Cassis amewakaribisha viongozi hao akiwemo rais wa Ukraine ambaye hata hivyo amehutubia kupitia ujumbe kwa njia ya vidio. Shirika moja maarufu lisilo la kiserikali nchini Uswisi limeikosoa nchi hiyo likiita ni eneo la kukimbilia kujificha matajiri wa kirusi kama ambavyo pia ni kituo cha biashara cha mafuta ya Urusi, nafaka na makaa ya mawe.
Uswisi yakosolewa
Shirika hilo linalojiita jicho la umma limewatolea mwito watendaji wakuu wenye maamuzi nchini Uswisi kutumia nafasi zao kusitisha ufadhili wa vitendo vya kimabavu vya ukatili dhidi ya ubinadamu vinavyofanywa na Urusi nchini Ukraine. Tamko hilo la shirika la public Eye limetolewa leo katika wakati rais Cassis wa Uswisi akiufungua mkutano wa kuisadia Ukraine ambao umehudhuriwa na maafisa wa serikali, mashirika ya harakati za kutetea binadamu, sekta binafsi, wasomi na mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema Umoja wa Ulaya utaunda jukwaa la kuratibu harakati za ujenzi mpya wa Ukraine baada ya vita na Urusi na jukwaa hilo litatumika kuonesha kinachohitajika katika uwekezaji, shughuli za uratibu na namna fedha zitakavyotumika. Von der Leyen amesema tangu mwanzoni mwa vita vya Ukraine, Umoja wa Ulaya umekusanya kiasi yuro bilioni 6.2 kuisadia nchi hiyo.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa upande wake amesema kuijenga upya Ukraine ni jukumu la kawaida la ulimwengu wote wa nchi zinazofuata demokrasia, akisisitiza kwamba kujengwa upya nchi yake iliyoharibiwa na vita kutaleta amani duniani kwa maneno mengine ni hatua kubwa ya mchango wa kuunga mkono amani duniani. Akaongeza kusema kwamba kuna kazi kubwa ya kufanyika.
"Ni muhimu sio tu kujenga upya vile vilivyoharibiwa na wavamizi bali pia kutengeneza misingi kwa ajili ya maisha yetu, kwa ajili ya Ukraine iliyo salama, ya kisasa na yenye viwango na isiyokuwa na vizingiti. Hili ni jambo linalohitaji uwekezaji mkubwa wa mabilioni, teknolojia mpya, mifumo bora na bila shaka mageuzi.''
Mpango wa Marshall wa kuijenga upya Ukraine ni mpango kama uliowahi kuanzishwa na Marekani wa kiuchumi wa kuliokoa bara la Ulaya baada ya vita vya pili vya dunia.
Fikra ya mpango wa Marshall ilianzishwa Juni mwaka 1947 wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani wakati huo George C Marshall alipohutubia hadhara katika chuo kikuu cha Harvard na kutangaza kwamba Ulaya inapaswa kupewa msaada mkubwa au ikabiliwe na mporomoko wa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mpango huo ukasainiwa kuwa sheria na rais Harry Truman mnamo mwezi Aprili 1948 na kutangazwa rasmi kuwa sera ya Marekani kuhusu msaada.