Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana Brussels
27 Juni 2014Ingawa kila kitu kinadhihirisha uamuzi wa kumteuwa Juncker kushika nafasi itakayoachwa na mwenyekiti wa sasa wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, utapitishwa katika mkutano huo wa kilele, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amepania kufanya kila awezalo kutetea msimamo wake kuhusu mustakbali wa Umoja wa Ulaya.
"Si haki kwamba viongozi waliochaguliwa wa serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya waachilie mbali haki yao ya kumteuwa kiongozi wa halmashauri kuu. Ni muongozo mbaya na anayechaguliwa pia hafai. Jean-Claude Juncker ni mshika bendera wa mradi wa kuuzidishia madaraka Umoja wa Ulaya na kuyapunguzia madaraka mataifa wanachama. Yeye si mtu anaefaa kuiongoza halmashauri hii." Anasema Cameron
Majadiliano moto moto yanategemewa
Waziri Mkuu huyo wa Uingereza ameonya majadiliano yatakuwa makali kuhusu kuteuliwa waziri mkuu huyo wa zamani wa Luxembourg. Hata hivyo, ukakamavu wa Cameron unalinganishwa na mbio za sakafuni, maana anaungwa mkono na Waziri Mkuu wa Hungary tu, Viktor Orban, katika madai yake dhidi ya Juncker.
Viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya, tangu wa mrego wa kihafidhina mpaka wa mrengo wa shoto, wanamuunga mkono Juncker. Walipofika katika ukumbi wa mkutano, hakuna yeyote aliyesema chochote kuhusu hilo - si Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na wala Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Wito wa mageuzi unapingwa na wahafidhina
Licha ya lawama na vitisho vinavyotolewa na Cameron, viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya wanahisi muhimu ni mkakati na sio kiongozi anayeusimamia. "Uingereza inauhitaji Umoja wa Ulaya, sawa na vile ambavyo Umoja wa Ulaya unaihitaji Uingereza," amesema Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Thorning-Schmidt.
Naye Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Elio Di Ripo, licha ya kukiri kwamba msimamo wa Uingereza unaeleweka na unastahiki sifa, lakini ameonya kwamba taifa hilo haliwezi peke yake "kuwazuwia wenzao 26 ambao wanamtaka Juncker."
Viongozi wa Social Democratic wakiongozwa na Rais Hollande wameelezea uungaji mkono wao kwa Juncker tangu mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, wanataka badala yake watu waregeze kamba katika baadhi ya masuala kama vile bajeti ili kuunga mkono uwekezaji na ukuaji wa kiuchumi. Lakini madai hayo yanakataliwa na wahafidhina wakiongozwa na Kansela Merkel.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef