Viongozi wa Ulaya na Afrika wakusanyika Brussels
17 Februari 2022Mahusiano kati ya mabara hayo mawili yameathiriwa na msururu wa matatizo: kuanzia mizozo kuhusu chanjo za virusi vya corona, hadi kupambana na uhamiaji haramu, wimbi la mapinduzi barani Afrika, na kuongezeka kwa ushawishi wa mamluki wa Urusi barani humo.
Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika – AU Rais wa Senegal Macky Sall anasema matarajio yao ya pamoja, Waafrika na watu wa Ulaya, kwa mkutano huo wa kilele, ni kufikia ushirikiano mpya, wa kisiasa na wenye mwelekeo zaidi wa vitendo.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambaye nchi yake inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, anataraji mkutano huo wa kilele wa kwanza wa pamoja tangu mwaka wa 2017 unaweza kutimiza ndoto yake kubwa ya kutengeneza Mwafaka Mpya na Afrika wa kiuchumi na kifedha.
Umoja wa Ulaya unalenga kuwashawishi viongozi 40 wa Afrika mjini Brussels kuwa Ulaya ndio ”mshirika wake wa kuaminika” kwa kutangaza mpango wa uwekezaji unaolenga kuhamasisha mchango wa euro bilioni 150 fedha za umma na kibinafsi kwa kipindi cha miaka saba ijayo.
Mkutano huo unakuja katika wakati ambao Afrika inakumbwa na wimbi la mapinduzi ya kijeshi na wakati Ethiopia ikikabiliwa na mzozo wa kivita. Burkina Faso mwezi uliopita ilijiunga na Guinea, Mali na Sudan kama nchi ya nne iliyofungiwa nje na Umoja wa Afrika baada ya wanajeshi wake kumuondoa rais madarakani. Nchi hizo nne hazijawakilishwa mjini Brussels.
Macron anatafakari kuwapeleka kwingine katika eneo la Sahel wanajeshi wa Ufaransa walioko Mali baada ya kuvunjika kwa mahusiano, na kumaliza operesheni ya miaka tisa ya kupambana na wanamgambo wa itikadi kali nchini humo.
Vita dhidi ya janga la Covid-19 pia inatarajiwa kuwa mada kuu. Afrika imekasirishwa na kile inaona kuwa ni usambazaji usio wa haki wa chanjo za virusi vya corona kote ulimwenguni na kuliacha nyuma bara hilo.
Umoja wa Ulaya umechangia zaidi ya dozi milioni 400 kupitia mpango wa kugawana chanjo wa Covax na umeahidi kuipa Afrika Zaidi ya dozi milioni 450 ifikapo katikati ya mwaka huu. Unasema utaongeza ufadhili ili kuisaidia mifumo ya afya barani humo kupata chanjo, na kuahidi euro bilioni moja ili kupiga jeki utengenezaji wa chanjo barani humo katika siku za usoni.
afp