Viongozi wa Udugu wa kiislamu wahukumiwa kunyongwa Misri
8 Septemba 2018Mahakama ya Misri imewahukumu adhabu ya kifo watu 75 wakiwemo viongozi mashuhuri wa kundi la kiislamu na kutoa adhabu ya kifungo jela kwa zaidi ya watu wengine 600. Watu hao wamehukumiwa kufuatia tuhuma za kuhusika katika maandamano ya mwaka 2013 yaliyoishia na mauaji ya mamia ya waandamanaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama. Kesi hiyo kwa ujumla imewahusisha kiasi watu 700 waliotuhumiwa kuhusika na makosa kadhaa ikiwemo mauaji hadi uchochezi wa ghasia wakati wa maandamano yaliyokuwa yanaungwa mkono na kundi la udugu wa kiislamu katika uwanja wa Rabaa Adawiya mjini Cairo.
Serikali inasema wengi wa waandamanaji walikuwa na silaha na kwamba wanajeshi wanane wa kikosi cha usalama waliuwawa.Awali ilitajwa na serikali kwamba zaidi ya polisi 40 waliuwawa.Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema kwamba zaidi ya waandamanaji 800 walipoteza maisha katika tukio moja la mauaji yaliyofanyika kwenye vurugu zilizofuatia harakati za mwaka 2011.Shirika la Amnesty International limelaani uamuzi wa Jumamosi uliochukuliwa na mahakama na kuitaja keso hiyo kuwa fedheha.
Mahakama ya jinai kusini mwa mji wa Cairo ilitangaza uamuzi wake leo wa kuwahukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa wengi wa viongozi maarufu wa kundi la udugu wa kiislamu akiwemo kiongozi wa juu wa kundi hilo Essam al-Erian sambamba na Mohammed Beltagi na ulamaa wa Safwat Higazi.
Kiongozi wa kidini wa kundi hilo la Udugu wa kiislamu Mohammed Badie pamoja na wanachama wengine wengi wa chama hicho kilichopigwa marufuku nchini Misri walihukumiwa kifungo cha maisha jela,kwa mujibu wa duru za mahakama.Wengine walioshtakiwa na kuhukumiwa walipata kifungo cha kuanzia miaka mitano hadi 15 jela.
Aidha watu watano waliokuwa pia wameshtakiwa kesi zao zilitupiliwa mbali kwasbabu walifariki wakiwa jela ingawa duru za mahakama hazikutowa maelezo zaidi ya ufafanuzi wa suala hilo. Kufuatia wiki kadhaa za maandamano mwaka 2013 ya kupinga kuondolewa madarakani kwa nguvu na jeshi rais Mohamed Mursi mwenye siasa kali,jeshi ambalo liliongozwa wakati huo na rais wa sasa Abdel Fatah al Sisi liliyavunja maandamano hayo kwa kutumia nguvu katika uwanja wa Rabaa.Waliwakamata mamia ya watu ambao walifunguliwa mashtaka ya uchochezi.mauji pamoja na kupanga maandamano haramu.
Mashirika la ya haki za binadamu yameikosoa kesi hiyo kwa kuwajumuisha waandamanaji walioshiriki kwa amani maandamano hayo pamoja na waandishi habari.Mwandishi habari mpiga picha maarufu aliyewahi kushinda tuzo aliyeripoti juu ya maandamano hayo Mahmoud Abu Zeid amehukumiwa kifungo cha miaka 5 jela lakini hivi karibuni ataachiwa huru kwa sababu ameshakaa muda mrefu jela.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/Reuters/AFPE
Mhariri:Zainab Aziz