Viongozi wa SADC kujadili masuala ya ulinzi na kiusalama
22 Machi 2024Hadi sasa ni mataifa machache tu kutoka katika eneo hilo ndiyo yaliyotuma vikosi vyake vya kulinda amani nchii Kongo, ikiwamo nchi jirani kwa pande zote mbili Tanzania iliyosema inashirikii mkutano huo kwa ukamifu wote.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje imesema Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazochangia vikosi vya kulinda amaniina dhima kubwa ya kuhakikisha utengamao katika eneo hilo inakuwa ni ajenda ya kudumu na kwamba inashiriki mkutano huu kikamilifu ukiwamo pia ule ulioanza jana ukiwahusu mawaziri wa mashauri ya kigeni. Mwezi uliopita, Tanzania iliungana na Malawi na Afrika Kusini kupitia kikosi maalumu cha kijeshi cha SADC na kupeleka wanajeshi Mashariki mwa DRC ikiwa na lengo la kurejesha amani na usalama katika eneo hilo.
Imefanya hivyo pia huko Msumbiji ambako wapiganaji wenye mafungamano na makundi ya kigaidi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara kaskazini mwa nchi hiyo tangu mwaka 2017.
Waziri wa mambo ya Nje wa Tanzania, January Makamba akizungumza siku moja kabla ya kuelekea katika mkutano huo alisema Tanzania itaendelea kutoa ushawishi wake kwa ajili kuyatafutia majawabu ya pamoja masuala tete yanayohusu amani na usalama katika eneo hilo. Ameongeza kwamba, "sauti yetu, kauli yetu, mkono wetu kauli ya mheshimiwa Rais, mkono wa mheshimiwa Rais umekuwa unahitajika".
Mkutano huo wa Lusaka ambao unafanyika katika wakati ambako wapiganaji wa M23 wakiendelea kuzidisha mashambulizi mashariki mwa Congo, utamulika kwa kina hali jumla ya mambo katika eneo hilo na kuanisha mikakati ya namna ya kuzidisha operesheni ya amani.Vikosi vya Msumbuji, Rwanda vyakomboa mji muhimu
Wachambuzi wa mambo wanasema ingawa kumekuwa na nchi chache zilizotuma vikosi vya kulinda amani kwenye maeneo yenye mizozo, bado viongozi wa Sadc wanaona haja ya kuendelea kuweka juhudi za kidiplomasia za pamoja ili nchi zilizotumbukia kwenye mizozo zinasuke. Majid Mjengwa ni mmoja wa wachambuzi wanatupia macho mizozo hiyo inayoendelea, "Viongozi wanapokutana katika tukio kama hilo la Lusaka linatoa nafasi kwa juhudi za kidiplomasia au diplomasia kuchukua mkondo wake kwa maana ya kujadili kwa kina changamoto zilizopo na namna gani ya kuzitatua."
Ripoti za hivi karibuni zinasema wanajeshi wa SADC pamoja na Jeshi la DRC (FARDC) wamekuwa wakipambana na waasi wa M23 hasa katika maeneo ya mji wa Sake ulioko kilometa 25 kaskazini magharibi mwa mji wa Goma.
Vikosi vya SADC vilichukua jukumu la kulinda amani kutoka kwa Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki, majuma kadhaa baada ya Rais wa DRC Felix Tshisekedi alipoamuru yaondoke akiyashutumu kushindwa kuwaondoa wapiganaji wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.
Na mkutano huo wa Lusaka unafanyika wakati baadhi ya nchi wanachama ndani ya jumuiya zote mbili yaani Sadc na ile ya Afrika Mashariki wakitupiana lawama wakituhumiana kuwaunga mkono waasi. Hali hiyo kama anavyoesema mchambuzi Mjengwa inapaswa kukemewa hadharani lakini vinginevyo mizozo na makundi ya waasi yanaweza kuendelea kuota mizozo katika eneo la kanda.
"Nani sasa anaweza akatoa tamko au kikao hicho kikatoa azimio la kushutumu nchi hiyo ambayo mwanachama wa jumuiya nyingine lakini inatuhumiwa …. Wafikie hatua ya kutamka, kulitamka jembe au koleo kwa jina lake kwa hiyo bila hivyo inaweza ikachukua muda mrefu zaidi kwa maana hawatakuwa wamefikia kwenye kiini cha tatizo," aliongeza Mjengwa.
Soma pia: SADC yazindua kituo cha kupambana na ugaidi
Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, mapigano yaliyozuka hivi karibuni mashariki mwa Congo, yamewalazimu watu 215,000 kukimbilia mjini Goma mji ambao tayari umekuwa ukielemewa na idadi kubwa ya wakimbizi. Na huko Msumbiji zaidi ya watu 700,000 wameyahama makazi yao katika Jimbo la Gabo Delgado tangu wapiganaji wa kigaidi waanzishe mashambulizi yao mwaka 2017, hali ambayo imelilazimu jeshi la Sadc kuongeza muda ya operesheni yake ya amani nchini humo.