Uamuzi wa Rais Trump wapingwa na viongozi wa nchi za Kiarabu
1 Aprili 2019Katika tamko la mwisho baada ya mkutano wao wa kilele kumalizika, viongozi hao wa Umoja wa Kiarabu walisema wanasisitiza kuwa milima ya Golan inayokaliwa na Israel ni eneo la Syria kulingana na sheria ya kimataifa, maamuzi ya Umoja wa Mataifa na ya Baraza la Usalama. Katibu mkuu wa jumuiya hiyo Ahmed Aboul Gheit amesema hoja ya rais Donald Trump ni batili, sio halali kabisa.
Rais Donald Trump alitia saini tamko la kuitambua milima ya Golan kuwa ni sehemu ya Israel wiki iliyopita. Israel iliiteka milima ya Golan wakati wa vita vya mwaka 1967 vya mashariki ya kati baada ya Syria kuitumia sehemu hiyo yenye umuhimu wa kijeshi, kwa ajili ya kushambulia sehemu za kaskazini mwa Israel. Israel ililiunganisha eneo hilo katika milki yake mnamo mwaka 1981.
Kwa muda wa miaka mingi nchi za kiarabu zimekuwa zinataka eneo hilo la milima lirudishwe kwa Israel na zimeulaani uamuzi wa rais Donald Trump wa kuitambua milima hiyo kuwa ni sehemu ya ardhi ya Israel.
Viongozi wa Kiarabu wamesema watawasilisha azimio kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya uamuzi wa Marekani na pia wameahidi kuwaunga mkono Wapalestina katika jitihada zao za kutaka uhuru wao.
Syria haikuwakilishwa katika mkutano huo kutokana na kusimamishwa uanachama wake tangu mwaka 2011 na hadi mkutano huo wa kilele ulipomalizika viongozi wa jumuiya hiyo ya nchi za Kiarabu hawakuwa wamefikia makubaliano juu ya kuiruhusu Syria kurejea kwenye jumuiya hiyo.
Mkutano huo ulifanyika wakati ambapo kuna misukosuko nchini Algeria, Sudan, na Yemen ambazo pia viongozi wake hawakuhudhuria mkutano huo wa kilele na Emir wa Qatari naye aliondoka mapema kutoka kwenye mkutano bila sababu kutolewa.
Vyanzo/AFP/DPA