Viongozi wa nchi za COMESA waanza mkutano Malawi
14 Oktoba 2011Wakati huohuo, Rais wa Sudan Omar al Bashir tayari amewasili tangu jana usiku nchini Malawi kukihudhuria kikao hicho cha COMESA. Itakumbukwa kuwa Rais Bashir anasakwa na mahakaama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC .
Bashir na ujumbe wake wa watu 26 walikaribishwa nchini Malawi kwa ngoma za kitamaduni na kupewa ulinzi mkali na jeshi la nchi hiyo, kinyume na matakwa ya ICC ya kutaka rais huyo akamatwe na kukabidhiwa mahakama hiyo pindi atakapoonekana katika nchi zilizotia saini mkataba ulioiunda mahakama hiyo.
Waziri wa mambo ya kigeni nchini Malawi amesema nchi hiyo kamwe haitamkamata Rais Bashir kwa sababu kwanza, yuko nchini Malawi kama rafiki wa rais wa nchi hiyo Bingu wa Mutharika na pili ni kuhudhuria mkutano wa COMESA unaofanyika katika mji mkuu wa Malawi Lilongwe.
Hata hiyo mkuu wa sera za mambo ya nje wa umoja wa ulaya Catherine Ashton leo ameihimiza Malawi imkamate Bashir na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC: Ashton amesema malawi ni moja ya nchi zilizotia saini makubaliano ya kuundwa mahakama hiyo na ni lazima ishirikiane nayo katika kumkatama Bashir, mapema hapo jana shirika la kutetea haki za kibinaadam la Human rights watch pia lilitoa ujumbe kama huo.
Bashir ni rais wa kwanza aliye mamlakani aliyeshtakiwa rasmi na mahakama ya ICC iliyotoa warranti ya kukamatwa kwake kwa makosa ya mauaji ya halaiki, makosa dhidi ya haki za kibinaadam pamoja na makosa ya uhalifu wa kivita miongoni mwa mengine.
Nchi ambazo zimemruhusu rais Omar el bashir kuingia nchini mwao hata baada ya ilani ya kukamatwa kwake kutolewa na ICC mwaka wa 2009 ni Kenya, Djibouti na Chad. Itakumbukwa pia Juni mwaka huu Bashir alisafiri kuelekea Uchina. Afrika kusini tayari imeshatoa ripoti ya kusema kuwa pindi El Bashir atakapoingia nchini humo atakamatwa na kukabidhiwa kwa ICC.
Kila safari ya Bashir na hasa katika mataifa yaliotia saini mkataba ulioiunda mahakama ya ICC, kama Kenya, Uturuki, Zambia na Malaysia, mahakama hiyo imekuwa ikiiarifu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambalo bado linajadili hatua ya kuchukua dhidi ya kiongozi huyo wa Sudan.
Leo nchi 19 wanachama wa COMESA wamekutana pamoja ili kujadili uwezekano wa kuwa na soko moja la kufanya biashara barani Afrika ifikapo mwaka wa 2012. Huu ni mkutano wa saba wa COMESA ambapo wafanyabiashara na viongozi wanazungumzia mikakati muhimu ya kukuza sayansi na teknologia kwa ajili ya kukuza biashara barani Afrika.
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Issayas Afweki wa Eritrea, Pierre Nkurunzinza wa Burundi na King Mswati wa tatu wa swaziland ndio miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mkutano wa COMESA.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFPE
Mhariri: Saumu Mwasimba