Mkutano juu ya mgogoro wa Zimbabwe.
18 Agosti 2008Viongozi wa nchi za kusini mwa Afrika wameshindwa kuwaleta pamoja rais Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai ili wapatane juu ya kugawana mamlaka.
Hatahivyo matumaini ya kufikia suluhisho nchini Zimbabwe bado yapo.
Mkutano wa viongozi wa nchi za jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC uliomalizika mjini Johannesburg ulishindwa kuzipatanisha pande za serikali na upinzani juu ya kugawana mamlaka nchini Zimbabwe.
Rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani M.Tvsangirai pia walihudhuria mkutano huo ambapo mpatanishi rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini alikuwa na matumaini ya suluhisho kufikiwa. Hatahivyo Mbeki amesema mazungumzo yataendelea.
Rais Thabo Mbeki pia ameitaka jumuiya ya kimataifa iwe na subira na isijiingize katika mgororo wa Zimbabwe.
Rais Mugabe na kiongozi wa upinzani hawakuweza kukubaliana juu ya kugawana mamlaka katika serikali ya umoja nchini Zibmabwe. Pande mbili hizo bado hazijafikia ufafanuzi juu ya madaraka ya rais na ya waziri mkuu. Hatahivyo waziri wa mambo ya nje wa Angola aliehudhuria mkutano wa mjini Johannesburg Joao Miranda amesema tofauti zilizobakia ni ndogo. Lakini pia amesema kwamba Mugabe na Tvsangirai bado wanatofautiana juu ya suala la mamlaka ya kiutendaji.
Mjumbe aliekaribu na rais Mbeki amesema miongoni mwa masuala magumu ni iwapo rais Mugabe atakuwa na mamlaka ya kuwateua na kuwafukuza mawaziri, na kwa muda gani serikali ya mpito itakuwa madarakani.
Chama cha upinzani kinataka kuwepo kwa ibara itakayoeleza wazi kuwa ,ikiwa upande mmoja utajitoa kwenye serikali, lazima uchaguzi ufanyike mnamo kipindi cha siku 90.
Kiongozi wa upinzani Tsvangirai anaamini kuwa ana haki ya kuwa na mamlaka makubwa zaidi kutokana na kushinda katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa rais. Lakini chama kinachotawala Zanu PF. kinasema Mugabe lazima atambuliwe kuwa rais kutokana na kushinda uchaguzi wa raundi ya pili ambapo chama cha upinzani hakikushiriki.
Akizungumza baada ya mkutano huo katibu mkuu wa chama cha upinzani MDC,bwana Tendai Biti amesema pana ulazima wa kufikia suluhisho haraka. Amesema upande wa upinzani una dhamira ya kweli katika kuutatua mgogoro wa Zimbabwe.