Kikosi cha Sahel chapiga hatua muhimu, chahitaji fedha zaidi
16 Februari 2021Rais wa Mauritania Mohammed Ould Ghazouani amesema wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa viongozi wa ukanda huo, kuwa kikosi cha pamoja cha jeshi cha nchi wanachama wa muungano wa Sahel G5- Mali, Niger, Chad, Burkina Faso na Mauritania kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhoofisha makundi ya ugaidi katika ukanda huo.
Ghazouani ameongeza kuwa kikosi hicho cha pamoja kimezidisha oparesheni zake katika eneo hilo huku makundi ya kigaidi yakipata hasara kubwa.
Wakati huo huo, Rais wa Chad Idriss Deby na mwenzake wa Ghana Nana Akufo-Addo wametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kupanua oparesheni ya vikosi vyake vya kulinda amani hadi katika ukanda huo.
Soma zaidi: Shambulizi la kigaidi lawauwa watu 56 Niger
Rais Deby amesema Chad itatuma wanajeshi 1,200 kupambana na wanamgambo katika eneo la mpakani wakati Ufaransa ikitazamia kupunguza idadi ya wanajeshi katika ukanda huo.
Deby amesema "Hali ya usalama inaendelea kutia wasiwasi. Athari za vitisho kutoka makundi ya kigaidi zimeongezeka kutoka ziwa Chad hadi eneo la Sahelo-Sahara."
Rais wa Nigeria Mahamadou Buhari amewaambia waandishi habari kuwa ukanda wa Sahel ulikabiliwa na "mwaka mbaya" 2020 kutokana na janga la Covid-19 na kushadidi kwa mashambulizi ya kigaidi.
Ujerumani na Ufaransa ni washirika muhimu wa Sahel
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, wanaowakilisha washirika muhimu wa Sahel, wanatarajiwa kujiunga na mkutano huo kwa njia ya video.
Jeshi la Ujerumani Bundeswehr, ambalo ni sehemu ya vikosi vya kulinda amani nchini Mali, pamoja na jeshi la Ufaransa yanaunga mkono muungano wa G5 katika oparesheni zao dhidi ya ugaidi.
Hata kabla ya kuanza kwa mkutano huo, tayari Mali ilikuwa inadai fedha zaidi kwa ajili ya kupiga jeki mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo hilo. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Mali Boubacar Gouro Diall ameliambia shirika la habari la DPA kuwa "Kikosi cha pamoja kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha. Ni muhimu kuwa ahadi walizotoa washirika wetu zinatimizwa."
Ukanda wa Sahel ambao upana wake unaanzia Chad katikati mwa bara Afrika hadi Pwani ya Magharibi mwa bara hilo umekumbwa na mashambulizi kutoka makundi mbalimbali ya kigaidi.
Baadhi ya makundi yanatajwa kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS au Al-Qaeda, ilhali makundi mengine ni ya waasi wa ndani.