1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G20 wawasili Bali kwa mkutano wa kilele

14 Novemba 2022

Viongozi kutoka mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani G20 wanaendelea kuwasili katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia leo kwa mkutano wa baada ya janga la UVIKO-19 uliotawaliwa na msuguano kati ya Marekani na China.

https://p.dw.com/p/4JT49
Indonesien Bali | Vorbereitungen G20 Gipfel
Picha: Willy Kurniawan/REUTERS

Mkutano huo wa G20 unatokea katika wakati ambapo watu kutoka kila pembe ya dunia wanakabiliwa na gharama kubwa ya maisha ikiwemo kupanda kwa bei za vyakula na mafuta, mzozo wa vita nchini Ukraine na tishio la matumizi ya silaha za nyuklia.

Mkutano huo unachukuliwa na wengi kama fursa adimu kwa viongozi wa G20 kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazozikabili dunia. Ni mkutano mkubwa zaidi wa viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda tangu kuanza kwa janga la ugonjwa wa UVIKO-19, hata hivyo sio mkutano wenye kupendeza.

Sunak anahudhuria mkutano wa G20 kwa mara ya kwanza

Ägypten | Der britische Premierminister Rishi Sunak in Ägypten
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: Stefan Rousseau/AP/picture alliance

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, ambaye anahudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, ametoa wito kwa mataifa yenye nguvu duniani kuungana dhidi ya unyonyaji wa uchumi wa dunia unaofanywa na wale aliowaita "watendaji wabaya."

Baada ya kuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Uingereza ndani ya mwaka mmoja, Sunak anatarajiwa kuwa na mkutano wake wa kwanza na Rais wa Marekani Joe Biden pamoja na viongozi wengine wa dunia katika mkutano wa kilele kisiwa cha Bali, Indonesia.

Soma zaidi: Mawaziri wa nje wa G20 kuanza mazungumzo, Bali

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ushindani kati ya China na Marekani umeongezeka kwa kasi. Beijing inaonekana kuwa na nguvu na yenye ushawishi na inapambana kwa udi na uvumbi kuwa taifa lenye nguvu kubwa duniani na kuchukua nafasi ya Marekani.

Mazungumzo ya leo ya ana kwa ana kati ya Biden na Xi pembezoni mwa mkutano huo, yana kumbukumbu kwa mbali kama mazungumzo ya vita baridi kati ya viongozi wa Marekani na muungano wa Sovieti huko Potsdam, Vienna ama Yalta ambayo yaliamua hatma ya mamilioni ya watu.

Biden kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Xi

Bildkombo Biden Xi Jinping
Picha: Rod Lamkey/CNP/picture alliance--Shen Hong/picture alliance/Xinhua

Biden amegusia kuhusu mkutano huo na Xi, na kutahadharisha juu ya kuvuka mstari mwekundu wa kila nchi kwa matumaini kwamba, ushindani kati yao hautakuwa chanzo cha nchi hizo mbili kuingia kwenye makabiliano na migogoro.

Mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani Jake Sullivan, amesema kuwa Biden atakuwa muwazi kwa Xi na anatarajia hilo pia kutoka kwa rais huyo wa China.

Maafisa wamesema, Biden ataisukuma China kuionya Korea Kaskazini ambaye ni mshirika wake, baada ya nchi hiyo kufanya majaribio kadhaa ya silaha zake za nyuklia.

Soma pia: G20: Mkutano wa kilele kujadili mazingira na Covid-19

Xi hata hivyo anatajwa kuwa huenda asiwe msaada mkubwa kwa Marekani. Anaingia kwenye mkutano huo na Biden baada ya kuchaguliwa kwa muhula wa tatu wa kihistoria hivi karibuni na kumfanya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi wa China.

Ama kwa upande wa Biden, ametiwa nguvu na habari kwamba chama chake cha Democrats kimeendelea kudhibiti baraza la Seneti baada ya kupata matokeo mazuri kuliko ilivyotarajiwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

Yumkini katika meza ya mazungumzo huko Bali nchini Indonesia, hatokuwepo Rais wa Urusi Vladimir Putin. Uvamizi wake wa kijeshi nchini Ukraine kumeifanya safari ya Bali kuingia doa. Badala yake, Putin amemtuma waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov kumwakilisha.

Vita vya nchini Ukraine au vitisho vya Putin vya kutumia silaha za nyuklia havimo kwenye ajenda kuu ya mkutano huo.