Viongozi wa dunia wampongeza Biden kujiondoa kwenye uchaguzi
22 Julai 2024Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ambaye amemuita Joe Biden, rafiki yake, amesema kiongozi huyo amefanikiwa kufanya mengi kwa nchi yake, Ulaya na Ulimwengu na uamuzi wake unahitaji kuheshimiwa.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemshukuru rais Biden kwa kile alichokiita,hatua kubwa alizochukuwa kuiunga mkono Ukraine,na kumsifu kwa uamuzi mgumu lakini thabiti wa kujiondowa katika kinyang'anyiro cha urais.
Waziri mkuu wa Poland Donald Tusk amempongeza rais Biden akisema maamuzi mengi magumu yaliyowahi kufanywa na kiongozi huyo wa Marekani, yamechangia kuifanya Poland, Marekani na Ulimwengu kuwa mahala salama na kuimarisha demokrasia, na hicho hicho anaamini ndicho kilichomsukuma kuchukua Uamuzi wake huu wa kutogombea muhula wa pili madarakani.
Soma pia:Biden ampendekeza Harris baada ya kujiondoa mbioni
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning amesema China haiwezi kutowa tamko lolote kuhusu hatua ya rais Joe Biden ya kutogombea muhula wa pili.
"Uchaguzi wa Marekani ni suala la ndani linaloihusu Marekani na sitotowa tamko lolote kuhusu hilo.''
Viongozi wengine wa dunia waliotoa pongezi ni pamoja na waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer na mwenzake wa Japan Fumio Kishida miongoni mwa wengine.