Viongozi wa dunia wampongeza Donald Trump
6 Novemba 2024Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kupitia ukurasa wake wa X amempongeza Trump kwa ushindi wake aliouita wa kihistoria. Amesema kurejea kwake katika ikulu ya White House ni mwanzo mpya kwa Marekani na kwa ushirikiano mkubwa kati ya Israel na Marekani.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema ataendelea kushirikiana na Marekani kwa manufaa ya raia wa nchi hizo.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Stammer amesema ana matumaini ya kufanya kazi na Trump katika miaka ijayo. Ameongeza kuwa kama washirika wa karibu nchi yake na Marekani zinasimama bega kwa bega katika kulinda maadili ya pamoja ya uhuru, demokrasia na biashara.
Soma zaidi: Trump ajitangaza mshindi wa urais Marekani
Kwa upande wake Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amempongeza Trump na kuweka wazi kuwa yuko tayari kufanya kazi pamoja kama ilivyokuwa katika miaka minne ya utawala wake.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte ametoa pia pongezi kwa Trump kwa kushinda uchaguzi huo. Amesena uongozi wa Trump utakuwa muhimu katika kuiimarisha Jumuiya hiyo.
Baada ya Trump kujitangaza mshindi mapema Jumatano, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesema Umoja wa Ulaya na Marekani zina ushirikiano wa muda mrefu na uhusiano wa karibu wa kihistoria.
Naye Rais wa Halmashauri ya umoja huo Ursula Von der Leyen ameeleza kuwa anatazamia kufanya kazi pamoja na Trump kwa mara nyingine ili kuendeleza ajenda muhimu ya kimataifa.
Soma zaidi:Uchaguzi wa Marekani: Nini kinatokea siku ya uchaguzi na baadae?
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema kuwa nchi yake inaendelea kutegemea ushirikiano wa Marekani na amempongeza Trump kwa ushindi wake mkubwa.
Kwa upande, ikulu ya Kremlin imesema Rais Vladmir Putin hana mpango wa kumpongeza Trump, huku ikiongeza pia kuwa Moscow haijaingilia uchaguzi wa Marekani.
Naye Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban ameutaja ushindi wa Trump kuwa mkubwa zaidi katika historia ya siasa za Marekani na kuwa unahitajika sana duniani.
Wengine waliotoa pongezi kwa Donald Trump ni pamoja na Waziri Mkuu wa India Narendra Mordi, Georgia Meloni wa Italia, Naibu wake Matteo Salvini, Kansela wa Austria Karl Nehammer na Geert Wilders wa Uholanzi.