Viongozi wa dunia wakumbuka mauaji ya Wayahudi
23 Januari 2020Viongozi na wawakilishi kutoka nchi zipatazo 50 watakusanyika katika kituo cha kumbukumbu ya mauji ya Wayahudi cha Yad Vashem kuhudhuria kongamano ambalo litasisitiza zaidi msimamo wa pamoja wa kupinga ongezeko la chuki na ghasia dhidi ya Wayahudi.
Wizara ya mambo ya nje ya Israel imesema Rais wa Israel, Reuven Rivlin ni mwenyeji wa kongamano hilo ambalo ni tukio kubwa la kisiasa kuwahi kufanyika tangu taifa hilo lilipoanzishwa mwaka 1948. Rivlin amesema ana matumaini kwamba ujumbe utakaotolewa utaifikia kila nchi duniani.
''Nina imani kwamba viongozi wote duniani watasimama pamoja, wataungana kupiga vita ubaguzi, chuki na ghasia dhidi ya Wayahudi. Hili litafanikiwa kwa kuzingatia demokrasia na maadili ya kidemokrasia. Huu ni wito unaotolewa wakati wetu, hii ni changamoto yetu, hili ni chaguo letu,'' alibainisha Rivlin.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, wa Urusi Vladmir Putin, mwanamfalme wa Uingereza Charles, Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence na marais wa Ujerumani, Italia na Austria ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria kongamano hilo. Marais wa Ufaransa, Ujerumani na Urusi wanatarajiwa kuhutubia katika kumbukumbu hiyo, orodha ambayo ilizua utata.
Rais Duda asusia kongamano
Rais wa Poland Andrzej Duda mahali ambako kambi ya Auschwitz iko amelisusia kongamano hilo kwa sababu Putin amealikwa na kupewa nafasi ya kuhutubia. Urusi na Poland zimekuwa katika mzozano kuhusu mchango wa kila upande kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Duda amesema alitakiwa kujumuishwa kwa sababu nusu ya wahanga milioni 6 wa mauaji ya Wayahudi walikuwa ni Wayahudi wa Poland.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliwakaribisha viongozi mbalimbali wanaowasili, akisema kuwa ni muhimu wakumbuke kule walikotoka na ni muhimu kuangalia pale walipofika sasa.
Redio ya Israeli imetangaza kuwa zaidi ya askari polisi 11,000 wamesambazwa mjini Jerusalem kwa ajili ya kusaidia kulinda usalama, huku njia kuu na maeneo mengi ya mji huo yakiwa yamefungwa.
Hata hivyo, waandaaji wa kongamano hilo wamekosolewa vikali kwa kushindwa kuwashirikisha waathirika wa mauaji ya Wayahudi na badala yake kuzingatia zaidi viongozi wanaohudhuria. Katika kulijibu hilo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy amesema kwamba ujumbe wake umegawa baadhi ya nafasi ili kuwaruhusu waathirika zaidi kuhudhuria.
Msemaji wa kituo cha Yad Vashem, Simmy Allen amesema watu wapatao 100 walionusurika na mauaji ya Wayahudi wanatarajia kuwa miongoni mwa watu 780 wanaohudhuria kongamano hilo. ''Kwa kweli tungependa kuona waathirika wengi zaidi wanahudhuria katika kongamano hili, lakini pia tunawashughulikia wageni 48 kutoka duniani kote,'' alifafanua Allen.
Kwa mujibu wa wizara ya fedha ya Israel, kati ya watu 192,000 walionusurika na mauaji ya Wayahudi, asilimia 16 wana umri wa miaka 90 au zaidi na 14,800 walifariki dunia mwaka 2019 pekee.
(DPA, AP, AFP, Reuters)