1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kihistoria wafanyika kati ya China na Taiwan

7 Novemba 2015

Viongozi wa China na Taiwan wamekutana hii leo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka sitini kwa mazungumzo ya kihistoria. Rais wa China Xi Jinping amekutana na mwenzake wa Taiwan Ma Ying-jeou.

https://p.dw.com/p/1H1YD
Picha: picture-alliance/AP Photo/W. Maye-E

Mazungumzo hayo kati ya Xi na Ma, ndiyo ya kwanza kati ya viongozi wa mataifa hayo mawili hasimu tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe China kukamilika mwaka 1949. Viongozi hao wawili walipeana mikono na kutembea pamoja kuingia katika hoteli ya kifahari mjini Singapore ambapo mkutano kati yao umeandaliwa.

Katika hotuba fupi kwa wanahabari kabla ya kuelekea kwa mkutano wa faragha na Ma, Xi amesema lengo la muda mrefu la China ni kuona utangamano kati yao na Taiwan na kusema China na Taiwan ni familia moja na hakuna nguvu zozote zinazoweza kuwatenganisha.

Ma: Amani itawale

Rais wa Taiwan Ma Ying-Jeou amesema anatumai China itatumia amani na sio nguvu kutatua tofauati zilizopo kati yao, na kuongeza watu wa Taiwan wanatiwa wasiwasi zaidi na usalama na hadhi ya kisiwa chao.

Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Taiwan Ma Ying-jeou
Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Taiwan Ma Ying-jeouPicha: Getty Images/AFP/R. Rahman

Kiongozi huyo wa Taiwan amezitaka pande zote mbili kuheshimu misingi, maadili na mfumo wa maisha wa upande mwingine. Wakosoaji wa Ma wana mashaka kuwa mkutano kati yake na Xi utatoa fursa kwa China kukidhibiti kisiwa hicho.

Wengi wa raia wa Taiwan inayozingatia demokrasia wangependa kudumisha uhuru wao na kuendesha mambo yao kivyao baada ya kujitenga na China zaidi ya miongo sita iliyopita lakini China imekuwa ikisisitiza kuwa hatimaye pande hizo mbili ziungane.

Viongozi hao wawili kila mmoja anatumai kuwa ataandikisha historia ya kuwa alisaidia kumaliza uhasama na mgawanyiko huo wa miongo mingi kati ya China na Taiwan na kufikia makubaliano yanayoheshimika na kukubaliwa na kila upande.

Tangu Ma kushinda uchaguzi mwaka 2008, kumekuwa na hatua za maridhiano kati ya China na Taiwan huku kukiwa na makubaliano 23 ya kibiashara na ya kiufundi ambayo yamefikiwa kati yao.

Licha ya kuwa mkutano wa leo hautarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika uhusiano wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili, mkutano huo unaonekana kuusogesha mbele uhusiano kati ya China na Taiwan.

Taiwan kufanya chaguzi mwakani

Ma anatarajiwa kuondoka madarakani mwakani baada ya kuhudumu kwa mihula miwili. Uchaguzi mkuu unapangiwa kufanyika mwezi Januari. Amekanusha madai kutoka kwa wakosoaji wake kuwa mkutano na Xi unanuia kuathiri chaguzi zijazo.

Raia wa Taiwan wakiandamana kuupinga mkutano kati ya Xi na Ma
Raia wa Taiwan wakiandamana kuupinga mkutano kati ya Xi na MaPicha: Reuters/P. Chuang

Waandamanaji wachache walikusanyika nje ya majengo ya bunge ya Taiwan kupinga mkutano huo kwa sababu wanaamini utapelekea Taiwan kuwa chini ya himaya ya China.

Pande zote mbili zimesema hakuna makubaliano yoyote yatakayotiwa saini hii leo wala viongozi hao hawatatoa taarifa ya pamoja kwa waandishi wa habari.

Mara ya mwisho viongozi wa pande hizo mbili walikutana ilikuwa mwaka 1945, wakati kiongozi wa kikomunisti Mao Zedong alipokutana na Rais wa mfumo wa utawala wa kizalendo China Chiang Kai-shek katika jaribio la kufikia maridhiano ambayo hayakufanikiwa.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/ap/dpa

Mhariri: Bruce Amani