Viongozi wa ASEAN wakwepa kuikaripia China
8 Septemba 2016Lakini hata kabla ya taarifa hiyo kutolewa China imeeleza hali ya kuvunjwa kwake moyo na nchi nje ya eneo hilo kuingilia kati katika mvutano huo kuhusiana na eneo hilo la ujia huo wa maji baharini.
Viongozi wa nchi 10 za mataifa ya kusini mashariki mwa bara la Asia , pamoja na rais wa marekani Barack Obama na waziri mkuu wa China Li Keqiang miongoni mwa viongozi wengine sita , wamesisitiza umuhimu wa kulinda amani , uthabiti, usalama na uhuru wa safari za majini ndani na juu ya anga ya bahari ya kusini mwa China.
Lakini mswada wa taarifa itakayotolewa mjini Vientiane , Laos , umekwepa kwepa na kuzunguka mivutano ya kanda hiyo inayosababishwa na madai ya nchi kadhaa kudai eneo hilo muhimu katika bahari.
"Viongozi kadhaa wanaendelea kuwa na wasi wasi mkubwa kuhusiana na hali ya mambo katika bahari ya kusini mwa China," umesema mswada huo wa taarifa.
Obama aweka wazi suala la bahari
Lakini rais Barack Obama akihudhuria mkutano huo kama mgeni mualikwa aliliweka wazi suala hilo katika mkutano huo leo wakati ikiwa dhahiri kwamba wengi wa viongozi walioko katika mkutano huo hawataweza kuikaripia China na watatoa maelezo ya juu juu tu kuhusiana na kujipanua kwake katika eneo hilo la maji lenye utajiri mkubwa wa mali.
Obama alisema.
"Kuhusiana na suala la baharini tutaendelea kufanyakazi kuhakikisha kwamba mizozo inatatuliwa kwa amani , ikiwa ni pamoja na katika eneo la bahari ya kusini mwa China. Hukumu ya mahakama ya upatanishi mwezi Julai ambayo ni lazima itekelezwe, imesaidia kufafanua haki ya bahari katika eneo hilo.
Majadiliano ni muhimu
Natambua kwamba hii inaleta hali ya wasi wasi , lakini nina shauku ya kulijadili kuona tutakavyoweza kusonga mbele kwa pamoja kupunguza wasi wasi na kuhimiza diplomasia na uthabiti wa eneo lote."
Marekani imekuwa mara kwa mara ikielezea kuhusu wasi wasi wa hatua zinazochukuliwa na China katika bahari ya kusini mwa China. China imechukua maeneo ya kina kifupi katika habari hiyo na miamba ya matumbawe na kutengeneza visiwa na kujenga viwanja vidogo vya ndege vyenye uwezo wa kuhudumia ndege za kijeshi katika maeneo matatu .
Viongozi wa ASEAN katika mkutano wao wa awali siku ya Jumanne walieleza wasi wasi wao kuhusu China kujenga visiwa hivyo.
Wakati huo huo rais Barack Obama na kiongozi wa Ufilipino rais Rodrigo Duterte walikutana katika mkutano ambao sio rasmi jana Jumatano kabla ya kuhudhuria chakula cha usiku kwa ajili ya viongozi wanaohudhuria mkutano huo, wamesema maafisa wa Ufilipino.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / afpe / dpae
Mhariri: Yusra Buwayhid