1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa ASEAN kuafikiana juu ya mkataba wa RCEP

Sylvia Mwehozi
4 Novemba 2019

Thailand imesema kwamba nchi za ukanda wa Asia zimekuwa na mazungumzo kamili  juu ya kile kinachotazamiwa kuwa mkataba mkubwa wa kibiashara duniani wa RCEP.

https://p.dw.com/p/3SQRd
Thailand ASEAN Summit
Picha: picture-alliance/AP/S. Lalit

Nchi za ukanda wa Asia zinatarajia kutangaza makubaliano ya msingi ya mkataba wa Ushirikiano mpana wa Kiuchumi wa Kikanda - RCEP siku ya jumatatu, unaoungwa mkono na China na mataifa 16. Waziri wa biashara wa Thailand Jurin Laksanawist alisema kwamba, "kutakuwa na tangazo la pamoja juu ya mafanikio ya makubaliano ya RCEP kutoka kwa viongozi. India ni sehemu ya haya na tutatoa kauli ya pamoja".

Mkataba wa RCEP unajumuisha mataifa 10 ya ASEAN pamoja na China, Korea Kusini, Japan, India, Australia na New Zeland na unatarajiwa kutiwa saini mwaka 2020, kulingana na rasimu ya taarifa ya viongozi wa ASEAN. Mkataba huo unasubiriwa kwa hamu na China inayotazamiwa kupunguza makali ya vita vya kibiashara baina yake na Marekani. Mkataba huo unatarajiwa kutiwa saini mwakani huko Vietnam ambayo itakuwa mwenyekiti wa ASEAN.

Rais Donald Trump ambaye hakuhudhuria mkutano wa kilele wa ASEAN, ametuma mwaliko kwa viongozi hao katika "mkutano maalumu" nchini Marekani mapema mwaka ujao. Kukosekana kwa Trump katika mkutano huo, kuliacha mwanya kwa China na nchi nyingine zilizo na nguvu kikanda kuonyesha mwamba wake.

Thailand Asean-Gipfel l UN-Generalsekretär Guterres und der thailändische Premierminister Chan-ocha
Katibu mkuu wa UN Antonio Guterres na waziri mkuu wa Thailand Prayuth Chan-ocha(kulia)Picha: picture alliance/AP/W. Wanichakorn

Mshauri wa usalama wa ndani Robert O'Brien ambaye alimwakilisha Trump, amekutana na viongozi wa Jumuiya hiyo pembezoni mwa mkutano wa ASEAN siku ya Jumatatu..

"Beijing imetumia vitisho kujaribu na kuzuia mataifa ya Asean kutumia rasilimali zao za pwani, kuzuia upatikanaji wa dola trilioni 2.5 katika akiba ya mafuta na gesi peke yao. Mbinu hizi zinaenda kinyume na sheria za kimataifa na usawa. "

Ni waziri mkuu wa Thailand Prayuth Chan-cha na mawaziri wakuu wa Vietnam na Laos waliohudhuria mkutano huo pamoja na mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya ASEAN waliotumwa na viongozi wao.

India ina wasiwasi kwamba biashara zake ndogo zitaumizwa na wimbi la bidhaa nafuu kutoka China. Waziri mkuu wake Narendra Modi, aligusia wasiwasi huo hapo jana katika mkutano wa ASEAN akisema suala ambalo halijapatiwa ufumbuzi "ni upatikanaji wa soko la maana kwa pande zote". Beijing inautizama mkataba huo kama msingi wa mkakati wa biashara yake na mataifa jirani ya Asia na ambao unaungwa mkono na viongozi wa jumuiya ya ASEAn inayowakilisha soko la watu milioni 650.