1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika, Ulaya wabishania udhibiti chanjo za COVID-19

18 Februari 2022

Viongozi wa Afrika na Ulaya wanakamilisha hivi leo mkutano wao wa kilele ulioanza jana mjini Brussels, Ubelgiji, huku pande hizo mbili zikivutana juu ya chanjo ya COVID-19.

https://p.dw.com/p/47DzZ
Belgien Brüssel | EU-Afrika-Gipfel | Cyril Ramaphosa, Charles Michel und Emmanuel Macron
Picha: Olivier Hoslet/AFP/Getty Images

Kwenye mazungumzo yao ya Alkhamis (Februari 18), siku ya ufunguzi wa mkutano huo wa kilele mjini Brussels, viongozi wa Kiafrika walishinikiza kusitishwa kwa udhibiti wa hatimiliki za chanjo za ugonjwa wa COVID-19, wakisema hiyo ni fursa ya Ulaya na Afrika kudumisha mahusiano yao.

Rais Mokgweteesi Masisi wa Botswana aliwaambia waandishi wa habari kwamba hilo ni jambo ambalo lina nafasi kubwa kwenye mazungumzo ya Afrika na Ulaya na kwamba wao kama viongozi wa Kiafrika wangelipa umuhimu wake.

Wakiwa wamefadhaishwa na kiwango cha chini cha chanjo kwa raia wao, viongozi hao wa Kiafrika wamekuwa wakitowa wito kila mara kwa hakimiliki za chanjo kuondolewa ili mataifa masikini yaweze kuzalisha chanjo zao wenyewe.

Rais Samia ataka kiwanda cha chanjo

Belgien, Brüssel | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin von Tansania in Brüssel
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania (kushoto) akizungumza na Sudi Mnette wa Idhaa ya Kiswahili ya DW mjini Brussels, Ubelgiji.Picha: Mohammed Khelef/DW

Siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania aliiambia DW mjini Brussels kuwa nchi yake inataka kuanzisha kiwanda chake cha kutengeneza chanjo lakini lazima mataifa ya Ulaya yashawishi wenye hakimiliki za chanjo kuwachia huru haki hizo.

Serikali za mataifa yanayoendelea zimekuwa zikizilaumu Marekani na Umoja wa Ulaya kwa kushikilia chanjo za COVID-19 pamoja na teknolojia nzima ya chanjo katika kipindi chote cha janga hilo la kilimwengu.

Kwa sasa ni asilimia 12 tu ya wakaazi wa bara la Afrika waliochanjwa kikamilifu ikilinganishwa na asilimia 71 barani Ulaya.

Umoja wa Ulaya unakanusha ukosowaji dhidi yake, ukisema umechangia takribani dozi milioni 145 kwa bara la Afrika, huku ukidhamiria kufikisha dozi milioni 450 kwenye majira ya kiangazi ya mwaka huu, 2022. 

Ulaya yawekeza Afrika

Belgien Brüssel | EU-Afrika-Gipfel | Ursula von der Leyen und Macky Sall
Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen (kushoto) na Rais Macky Sall wa Senegal.Picha: John Thys/AFP/Getty Images

Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, pia alisifia uwekezaji wa Umoja wa Ulaya kwenye viwanda vya chanjo nchini Senegal na Rwanda.

Mnamo Oktoba 2020, India na Afrika ya Kusini zilipendekeza kusitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Hakimiliki za Kibiashara, TRIPS, katika teknolojia ya matibabu yanayohusiana na COVID-19 katika Shirika la Biashara Ulimwenguni, WTO, lakini zikakumbana na kigingi cha mataifa ya Magharibi.

Zaidi ya viongozi 40 wa Afrika wamekuwa wakikutana na wenzao wa Umoja wa Ulaya tangu jana mjini Brussels. 

Umoja wa Ulaya umesema utatowa kitita cha euro bilioni 300 kusaidia sekta ya afya, elimu na uthabiti barani Afrika kukabiliana na mradi wa China uitwao Belt and Road Initiative.