1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika kuzindua kanda mpya ya soko la pamoja

10 Juni 2015

Viongozi mataifa 26 ya Kiafrika wanakutana Misri hii Jumatano (10.06.2015) kusaini makubaliano ya kuanzisha soko la pamoja litakalojumuisha nusu ya bara la Afrika na kuwahudumia watu milioni 625.

https://p.dw.com/p/1FeL0
African Union Development Planning in Abidjan
Picha: Getty Images/Afp/Issouf Sanogo

Kusainiwa makubaliano hayo ya biashara huru kati ya jumuiya tatu TFTA, kunahitimisha majadiliano yaliyodumu miaka mitano yenye lengo la kuunda mfumo wa ushuru wa upendeleo ambao utarahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka mataifa wanachama.

Hafla ya kusainiwa makubaliano hayo inafanyika katika mkutano wa kilele uliyoitishwa na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi katika eneo la mapumziko la Sharm el-Sheikh, ambako wajumbe wa majadiliano walikamilisha kuratibu mswada wa makubaliano hayo wiki hii.

Makubaliano hayo yanajumlisha maslahi ya jumuia ya Afrika Mashariki EAC, jumuiya ya maendeleo ya mataifa ya kusini mwa Afrika SADC, na jumuiya ya soko la pamoja la mataifa ya mashariki na kusini mwa Afrika COMESA, ambazo mataifa yake yana pato la jumla la ndani la dola trilioni moja.

Sharm el-Sheikh, EAC, SADC, COMESA, Egypt, Africa
Mwenyeji wa Mkutano wa Sharm el-Sheikh, rais Abdul-Fattah al-Sisi.Picha: El-Shahed/AFP/Getty Images

Utatuzi wa migogoro ya kibishara

Wanachama wa jumuiya hizo wanaanzia kwenye mataifa yenye kiwango fulani cha maendeleo kama vile Afrika Kusini na Misri hadi mataifa kama Angola, Ethiopia na Msumbiji, ambayo yanatazamwa kama mataifa yenye uwezo mkubwa wa ukuaji wa kiuchumi.

Wajumbe wa majadiliano wanasema makubaliano hayo yameshughulikia wasiwasi kama vile utatuzi wa migogoro ya kibiashara na ulinzi wa viwanda vidogo vidogo pale mkataba huo wa TFTA utakapoanza kutekelezwa.

Waziri wa viwanda na biashara wa Misri Mounir Fakhri Abdel Nour, alisema ratiba ya kuondoa vikwazo vya kibiashara bado haijafanyiwa kazi, na kwamba makubaliano hayo yatapaswa kuridhiwa na mabunge ya mataifa wanachama katika kipindi cha miaka miwili.

Maafisa wamesema mkataba huo wa TFTA unalenga hatimaye kuziunganisha pamoja kanda hizo tatu, lakini kwamba makubaliano kati ya mataifa yataendelea. " Lengo la mwisho ni kurahisisha usafirishaji wa bidhaa katika mataifa hayo bila ushuru," alisema Peter Kiguta, Mkurugenzi mkuu wa jumuya ya Afrika Mashariki.

Ulimwengu wa kibiashara wayakaribisha

Pamoja na kuwepo mashaka, mkataba wa TFTA umepokelewa vyema na viongozi wa biashara duniani, huku wataalamu wakibainisha kuwa ni asilimia 12 tu ya biashara ya Afrika inayofanyika baina ya mataifa barani humo.

Baadhi ya wakuu wa mataifa wanachama wa TFTA.
Baadhi ya wakuu wa mataifa wanachama wa TFTA.Picha: picture alliance/dpa/Gcis/Siyasanga Mbambani

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na Maendeleo ulisema mwaka 2013 kuwa ikiwa Afrika inataka kuimarisha biashara yake ya ndani, laazima ijikite katika kuunda nafasi zaidi kwa sekta binafsi kuchukuwa jukumu kubwa zaidi.

Wachambuzi wanasema ingawa ukuaji wa bara hilo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita umezidi kiwango cha ongezeko la pato jumla la ndani la dunia kwa karibu asilimia tatu, lakini limekuwa likikabiliwa na kushuka kwa bei za bidhaa, ukosefu wa umeme, machafuko ya kisiasa na rushwa.

Waziri wa viwanda na biashara wa Misri Fakhri Abdel Nour amesema TFTA itasaidia kupanua soko la eneo hilo, kuimarisha ushindani na kuvutia uwekezaji kwa vile inajikita katika ujenzi w amiundo mbinu na uwezo wa uzalishaji.

Jumuiya ya biashara itanufaika hasa na kuboreka kwa mfumo wa biashara,ambao unapunguza gharama za biashara na kufutwa kwa sheria kinzani za biashara.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Hamidou Oummilkheir