1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Vikosi vya Urusi vyasonga mbele mashariki mwa Ukraine

Hawa Bihoga
17 Februari 2024

Wizara ya Ulinzi Urusi imesema vikosi vyake vimesonga mbele kwenye uwanja wa mapambano katika maeneo manne tofauti ikiwa ni pamoja na kwenye mji wa kimkakati wa Avdiivka uliopo mkoa wa mashariki mwa Ukraine wa Donetsk.

https://p.dw.com/p/4cWpX
Ukraine | Avdiivka
Mapambano ya kuwania mji wa mashariki mwa Ukraine wa AvdiivkaPicha: Elif Kizil/Anadolu/picture alliance

Ukraine ilitangaza mapema hii leo kuviondoa vikosi vyake kutoka mji huo, hatua iliofungua njia kwa vikosi vya Urusi kusonga mbele zaidi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwezi Mei mwaka jana ilipoukamata mji wa Bakhmut baada ya mapigano makali.

Maafisa kutoka pande zote za mzozo wanasema vita katika mji wa Avdiivka vimegharimu maelfu ya maisha, ingawa hadi sasa hakuna upande uliotoa idadi ya vifo na majeruhi.

Tathmini za kijasusi za mataifa ya Magharibi, zinaonesha kuwa maelfu ya wanaume kutoka Urusi na Ukraine waliuwawa katika mapigano hayo.

Mji wa Avdiivka ni ufunguo kwa lengo la Moscow kuchukua udhibiti kamili wa mikoa miwili ya Mashariki mwa Ukraine ya Donetsk na Luhansk, ambayo ni sehemu ya minne ambayo Urusi inasema imeitwaa lakini haina udhibiti kamili.