Vikosi vya Syria vyashambulia Mashariki mwa Ghouta
19 Februari 2018Ndege za kivita za Syria leo zimefanya mashambulizi mapya Mashariki mwa Ghouta-eneo linaloshikiliwa na waasi. Hii ni baada ya uimarishwaji wa utawala na baada ya kutokea ishara ya uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya ardhini kufuatia roketi zilizofyatuliwa katika eneo hilo lililozingirwa.
Kulingana na kundi la waangalizi la haki za binadamu, watu 18 wameuawa leo kufuatia mashambulizi ambayo yamefanywa na vikosi vya Syria Mashariki mwa Ghouta. Kundi hilo limeongeza kuwa mashambulizi hayo pia yamewajeruhi watu na kusababisha uharibifu wa mali.
Watu tisa wamefariki katika mji wa Hammuriyeh Mashariki mwa Ghouta huku wengine tisa wakiuawa sehemu tofauti kufuatia mapambano hayo.
Eneo la Mashariki mwa Ghouta linaloshikiliwa na waasi tangu 2012, ndiyo sehemu iliyosalia mikononi mwa waasi karibu na Damascus, na rais wa Syria Bashar al-Assad amevipeleka vikosi vyake katika eneo hilo kwa lengo la kulikomboa eneo hilo.
Mazungumzo kuliondoa kundi la Hayat Tahrir al-Sham?
Kundi la waangalizi wa haki za kibinadamu la Syria limesema mazungumzo yamekuwa yakiendelea ya kuliondoa kundi la Jihadi liitwalo Hayat Tahrir al-Sham ambalo linadhibiti baadhi ya maeneo ya Mashariki mwa Ghouta japo halijajitanua sana, ili kuafikia maelewano.
Mkuu wa shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Uingereza Rami Abdel Rahman amesema kuwa kufeli kwa mazungumzo kungeashiria mwanzo wa mashambulizi.
Mapema mwezi huu, vikosi vya serikali vilifanya mashambulizi kwa siku tano mfululizo katika eneo hilo lililozingirwa na kusababisha vifo vya raia 250 na mamia ya watu walijeruhiwa. Tangu wakati huo, vikosi vya serikali vimeishambulia miji ya Mashariki mwa Ghouta, yakiwemo mashambulizi ya leo.
Kwa mujibu wa kundi hilo la waangalizi wa haki, serikali ilianza kuwapeleka wanajeshi Mashariki mwa Ghouta tarehe 5 Februari, siku ambayo pia ilianza mashambulizi makali ya siku tano mfululizo katika eneo hilo. Kundi hilo limeongeza kusema kuwa hapo jana Jumapili, vikosi vya serikali vilifyatua roketi 260 katika miji ya Mashariki mwa Ghouta. Mashambulizi hayo ya jana yalisababisha vifo vya raia 17.
Udhibiti wa Mashariki mwa Ghouta
Utawala wa Syria unadhamiria kuchukua udhibiti wa Mashariki mwa Ghouta ili kusitisha mashambulizi ya roketi ambayo yamekuwa yakifanywa na makundi ya waasi yakiulenga mji wa Damascus.
Katika tukio tofauti, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ameonya kuwa hatua yoyote ya vikosi vya Syria pamoja na wapiganaji wa Kikurdi kaskazini mwa Syria haitaizuia Uturuki kuendeleza mashambulizi yake ambayo sasa yamedumu kwa mwezi mmoja.
Cavusoglu alikuwa akizungumzia ripoti katika shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Syria SANA kuwa vikosi vinavyounga mkono serikali vilitarajiwa katika eneo la Afrin kukabili mashambulizi ya Uturuki dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi wa YPG.
Mwandishi: John Juma
Mhariri: Yusuf Saumu