1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya serikali ya Syria vyakaribia kudhibiti Aleppo

8 Desemba 2016

Naibu waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Ryabkov amesema kuwa Urusi inakaribia kuafikiana na Marekani kuhusiana na kusitishwa kwa vita katika mji wa Aleppo nchini Syria.

https://p.dw.com/p/2TwTg
Aleppo Syrien Ruinen Stadt
Picha: Reuters/A. Ismail

Serikali ya Syria na mshirika wake Urusi zilikataa miito ya awali ya kusitishwa kwa vita katika mji huo wa Aleppo na kuendeleza mashambulizi ya kijeshi ambayo yaliwalazimu waasi kutorokea katika maeneo mbali mbali. 
Vituo vya habari nchini Urusi hii leo vilimnukuu naibu huyo wa waziri wa mambo ya nje, Sergei Ryabkov akisema kuwa Urusi na Marekani zinakaribia kupata maelewano kuhusiana na Aleppo lakini akatoa tahadhari ya kutokuwa na matarajio makubwa .
Waziri wa masuala ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov walikutana hapo jana nchini Ujerumani lakini hawakutoa taarifa yoyote.
Baada ya mkutano huo, Kerry alisema kuwa wanatarajia kukutana tena hii leo kwa mkutano mwingine.
Kabla ya mkutano huo wa jana, Lavrov aliulizwa kuhusu kukubali kwa Urusi kusitisha mapigano hayo na akasema,“nakubaliana na nathibitisha kuunga mkono pendekezo lililotolewa na Marekani tarehe 2 mwezi Desemba,“ akitaja mkutano kati yake na Kerry mjini Rome ambapo walikubaliana kuhusu mpango wakuwaondoa raia na waasi kutoka Mashariki mwa Aleppo na pia kuhusu mpango mpya wa kusitisha mapigano.
Kulingana na shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao nchini Uingereza, raia 19 waliuawa katika mashambulizi yaliofanywa na majeshi ya serikali hapo jana. 

Syrien Flüchtende aus dem östlichen Aleppo
Raia wa Aleppo wahamia katika ngome inayodhibitiwa na serikali mjini humoPicha: Reuters/Sana

 Ushindi mjini Aleppo ni hatua muhimu katika kusitisha vita nchini Syria

Wakati huohuo, rais wa Syria Bashar al- Assad amesema kuwa ushindi wa jeshi lake mjini Aleppo utakuwa hatua kubwa sana katika kutamatisha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimedumu kwa miaka mitano nchini humo huku waasi katika mji huo wa pili mkubwa zaidi nchini Syria wakipoteza uthibiti wa mji huo.
Katika mahojiano na gazeti moja nchini humo, Assad aliongeza kuwa kuwafurusha waasi mjini Aleppo pekee hakutamaanisha mwisho wa vita.
Katika makabiliano ya wiki tatu, majeshi ya serikali ya Syria yameweza kudhibiti takriban asilimia 80 ya eneo la Mashariki la Aleppo ambalo limekuwa ngome ya waasi hao tangu mwaka 2012.
Mji wa Aleppo ulikuwa kitovu cha utamaduni na biashara nchini Syria lakini kuzuka kwa mapigano mjini humo miaka minne iliyopita kuliugawanya mji huo kati ya waasi katika eneo la Mashariki na majeshi ya serikali katika eneo la Magharibi. 
Rais Bashar al-Assad ameahidi kukabiliana na waasi hata baada ya Aleppo kukombolewa na kuongeza kuwa, vita nchini Syria havitafikia kikomo hadi pale kile alichokiita ''ugaidi'' kitakapoondolewa kabisa. 

Mwandishi: Tatu Karema/ape, afpe
Mhariri: Gakuba Daniel