Vikosi vya Kikurdi vyaanza kuondoka Manbij
3 Januari 2019Kiasi cha wapiganaji 400 wa Kikurdi wameshaondoka mjini Manbij hadi sasa, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Syria, inayosema kuwa kuondoka huko ni sehemu ya makubaliano waliyoyaita ya "kurejesha maisha ya kawaida kwenye eneo hilo la kaskazini mwa Syria."
"Vikosi vya Kikurdi vilijiondoa Manbij kaskazini mashariki mwa Aleppo kuelekea mashariki mwa Mto Euphrates." Ilisema taarifa iliyotangazwa na shirika la habari la Syria, ikiongeza kwamba msafara huo wa Wakurdi ulikuwa na magari zaidi ya 30.
Hata hivyo, shirika linalofuatilia haki za binaadamu la Syria limesema wapiganaji waliondoka ni 250, na waote wako chini ya uongozi wa kundi linaloungwa mkono na Marekani, Syrian Democratic Forces (SDF).
Serikali mjini Ankara, ambayo linawaona viongozi wa kundi hilo kuwa magaidi kutokana na mafungamano yao na waasi wa Kikurdi ndani ya ardhi ya Uturuki, imetishia kulivamia kijeshi eneo la kaskazini mwa Syria linaloshikiliwa na SDF na tayari imeshatuma vikosi na vifaa vyake huko.
Hatima ya SDF mashakani
Hatima ya SDF imekuwa mashakani tangu Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza mwezi uliopita kwamba anaviondoa vikosi vya nchi yaje kutoka Syria. Akizungumza kwenye Ikulu ya Marekani hapo jana, Trump alisema ingawa anataka kuwalinda Wakurdi, hawezi kuviacha vikosi vya Marekani nchini Syria milele.
"Syria ilishapotea zamani sana. Tunazungumzia mchanga na mauti. Hatuzungumzii kuhusu utajiri mkubwa uliopo," alisema Trump.
Ripoti za hivi karibuni zinasema kuwa Trump amepanga ratiba ya kipindi cha miezi minne ya kukamilisha hatua ya kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria, lakini hapo jana alisema itachukuwa muda mrefu kidogo, bila kutaja hasa ni urefu gani, japo alisema kuwa Marekani itaondoka Syria ikiwa madhubuti na ikiwa imeshinda.
Hapo awali, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alimwambia Rais Vladmir Putin wa Urusi kwamba ushirika wa mataifa ya Magharibi kwa Wakurdi wanaopambana dhidi ya wapiganaji wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu lazima udumishwe. Macron alimwambia Putin kwamba vita dhidi vya muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi hilo la kigaidi bado havijesha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kasri ya Elysee, Macron alisisitiza kwamba vikosi vya muungano wa washirika "hasa hasa Wakurdi lazima walindwe kwa kuzingatia kujitolea kwao kupambana dhidi ya magaidi."
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga