Vifo zaidi vya waandamanaji vyaripotiwa Myanmar
3 Machi 2021Milio ya risasi na sauti za waandamanaji wanaokabiliana na maafisa wa polisi zimetanda katika mji wa Yangon ambapo vikosi vya usalama vya Myanmar vilifyatua risasi na kuwaua zaidi ya watu 10 na kuwajeruhi wengine takriban 30 huku wengine wakiwa bado hawajitambui.
Video kutoka maeneo mbalimbali katika mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari vya Myanmar zinaonesha vikosi vya usalama vikiwapiga kwa manati waandamanaji, kuwafukuza na hata kuwashambulia kikatili wafanyakazi wa gari la kubeba wagonjwa.
Haya yanajiri siku moja baada tu ya mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi jirani za Kusini Mashariki mwa Asia kutoa wito wa kusitisha matumizi ya nguvu na kujitolea kuisaidia Myanmar katika kutatua mgogoro wao.
Hakuna maneno yanayoweza kuelezea hali na hisia za waandamanaji
Kulingana na walioshuhudia, vikosi vya usalama viliamua kutumia risasi za moto bila kutoa ilani katika maeneo ya miji kadhaa. Jeshi la Myamnar lilionekana kuamua zaidi kuliko hapo awali kumaliza maandamano dhidi ya mapinduzi ya Februari 1 yaliyoiondoa serikali iliyochaguliwa ya Aung San Suu Kyi.
Mwanaharakati wa vijana Thinzar Shunlei Yi ameliambia shirika la habari la Reuters kupitia programu ya kutuma ujumbe kuwa mauwaji hayo ni ya kutisha, na hakuna maneno yanayoweza kuelezea hali na hisia zao.
James Faani ni rais wa Kamati ya Wakimbizi wa jamii ya China.
"Hapa sisi ni wakimbizi na hatuwezi kufanya chochote. Lakini angalau tulitaka kuonyesha ushirikiano wetu kwa watu wa Myanmar ambao wanapinga mapinduzi haya ya kijeshi, kwa sababu tungependa kutoa maoni kwa jumuia ya kimataifa ili kitu kifanyike nchini Myanmar," alisema Faani.
Juhudi za kuwasiliana na Msemaji wa baraza la kijeshi linalotawala Myanmar hazikufaulu, hakupokea simu ili kutoa maoni yake kuhusu kadhia hiyo.
Papa Francis amesikitishwa na machafuko ya Myanmar
Kulingana na Mhariri wa Gazeti la Monywa Ko Thit Sar, Athari kubwa zaidi zimeshuhudiwa katika mji wa kati wa Monywa, ambapo watu watano, kati yao wanaume wanne na mwanamke mmoja waliuawa.
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesikitishwa na mapigano hayo na umwagaji damu na vifo na kuzitolea wito mamlaka zinazohusika kufanya mazungumzo ili kusitisha ukandamizaji na matumizi ya nguvu.
''Natoa rai pia kwa jumuia ya kimataifa kufanya kazi ili kuhakikisha kuwa matakwa ya watu wa Myanmar hayapaswi kuzuiliwa na vurugu. Wacha vijana wa ardhi hiyo wapewe tumaini la siku zijazo ambapo chuki na dhuluma hutoa nafasi kwa maridhiano. Hamu iliyoonyeshwa mwezi uliopita kwamba njia ya demokrasia iliyodumu katika miaka ya hivi karibuni Myanmar inaweza kuendelea kupitia ishara thabiti ya kuachiliwa kwa viongozi wa kisiasa waliofungwa," alisema Papa Francis.
Takriban watu 35 wameuawa tangu mapinduzi hayo yalipofanyika Februari Mosi.