1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifaru vya Urusi vyaivamia ardhi ya Ukraine

Daniel Gakuba
24 Februari 2022

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ametangaza kuwa Urusi imeanzisha uvamizi kamili dhidi ya nchi yake. Awali Rais Vradimir Putin alisema jeshi la Urusi litafanya operesheni maalum ndani ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/47W3r
Krim Militärfahrzeug Armyansk
Picha: REUTERS

Katika ujumbe aliouchapisha ukurasa wake wa mtandao wa twitter, waziri Dmytro Kuleba amesema, ''Putin ameanzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine. Miji yenye amani ya Ukraine inakabiliwa na mashambulizi.'' 

Waziri huyo ameongeza kuwa tukio hilo ni vita vya ukandamizaji, na kuapa kuwa Ukraine itajilinda na itashinda, na kuwakumbusha viongozi wa dunia kuwa wana wajibu na uwezo wa kumsimamisha Putin.

Picha za kamera za usalama zimeonyesha misafara ya magari ya kijeshi ya Urusi ikiingia kwenye ardhi ya Ukraine kutoka katika rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi.

Russland TV Ansprache Putin Militäroperation Ukraine
Rais Vradimir Putin wa Urusi amemtishia yeyote atakayejaribu kuzuia uvamizi dhidi ya UkrainePicha: Kremlin/AFP

Putin atoa onyo kali

Vikosi vya Urusi vimelenga vituo kadhaa ndani ya Ukraine, wakati huo huo Putin akitoa onyo kwa nchi zinazoweza kuingilia kati, akidai zitakabiliwa na athari ambazo hazijawahi kushuhudiwa.

Kabla ya mapambazuko leo Alhamisi, miripuko mikubwa ilisikika katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev na miji ya mashariki mwa nchi hiyo ya Kharkiv na Odesa.

Soma zaidi: Marekani, washirika waiwekea vikwazo zaidi Urusi

Katika mji wa Kiev kunashuhudiwa msongamano mkubwa wa magari ya raia wanaoukimbia mji huo, na jeshi la Urusi limedai kuwa limeviharibu vituo vyote vya Ukraine vya ulinzi wa anga na viwanja vyote vya jeshi la angani la nchi hiyo katika saa chache baada ya kuanza kwa uvamizi huu.

Ukraine | Ansprache Präsident Wolodymyr Selenskyj nach Ankündigung der russischen Militäroperation
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema taasisi za Ulinzi za Ukraine ziko kaziniPicha: Ukrainian Presidential Press Service/REUTERS

Zelenskiy awataka wananchi wa Ukraine kubakia watulivu

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ametangaza sheria ya mazingira ya vita, akisema Urusi inailenga miundombinu ya Ukraine, na kuwataka raia wake kubakia majumbani kwa utulivu. Zelenskiy ameongeza kuwa taasisi za ulinzi za Ukraine zinafanya kazi zikishirikiana na washirika wao.

''Muda mfupi uliopita nimezungumza na Rais Biden. Marekani iko tayari kuratibu msaada wa kimataifa. Leo, tunataka utulivu wa kila mmoja wetu, ikiwezekana tukisalia nyumbani, '' amesema Zelenskiy na kuongeza kuwa wanafanya kazi, jeshi linafanya kazi, sekta nzima ya ulinzi na usalama ya Ukraine inafanya kazi.'

Ukraine Konflikt | Luftangriff auf Tschuhujiw
Wanajeshi wa Ukraine wakimsaidia raia aliyejeruhiwa katika shambuliziPicha: Wolfgang Schwan/AA/picture alliance

Guterres amtaka Putin kusitisha uvamizi

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hiki ndicho kipindi kigumu kabisa tangu alipochukuwa wadhifa wake, na amemuomba rais Vradimir Putin wa Urusi kusitisha uvamizi huu, kwa maslahi ya ubinadamu.

Jeshi la Urusi limesema haliwalengi raia, bali miundombinu ya kijeshi kwa kutumia silaha za kisasa zenye uwezo wa kupatia shabaha bila kosa. Licha ya ahadi hiyo lakini, tayari zipo taarifa za vifo kutokana na uvamizi huu, ikithibitishwa kuwa raia watano wa Ukraine wamekwishauawa.

ape,rtre