Venezuela kuwashtaki Wamarekani kwa kupanga mapinduzi
7 Mei 2020Siku ya Jumatatu Venezuela ilitangaza kwamba imewakamata wanajeshi wawili wa zamani wa kikosi maalum cha Marekani kwa tuhuma za kujaribu kumuondoa madarakani Maduro katika operesheni iliyofadhiliwa na upinzani unaoungwa mkono na Marekani.
Maduro amesema Wamarekani hao wamekiri na wameshtakiwa na mwanasheria mkuu wa serikali ya Venezuela katika mahakama za kiraia za nchi hiyo na mchakato huo utazingatia haki.
"Hapa Venezuela watahukumiwa kwa kuzingatia haki zao zote. Hawa Wamarekani wameikuta Venezuela nyingine ambayo hawakuitarajia. Yenye taasisi imara na watu ambao wamewashangaza, jeshi imara lenye mshikamano, jeshi madhubuti la kiintelijensia. Wanaangaliwa vizuri na kwa kuheshimu utu wao," alisisitiza Maduro.
Washukiwa watambuliwa
Kiongozi huyo wa nchi ya Amerika ya Kusini iliyokumbwa na mzozo, amezionyesha pasi za kusafiria za Wamarekani hao waliotambuliwa kama Luke Denman, mwenye umri wa miaka 34 na Aairan Berry, mwenye miaka 41.
Jeshi la Marekani limethibitisha kuwa Wamarekani hao ni wanajeshi wa zamani wa kikosi maalum cha jeshi la Marekani, Green Berets ambao walipelekwa Iraq.
Rais wa Marekani, Donald Trump amekanusha madai ya utawala wake kuhusika kwenye jaribio hilo na amemshutumu Maduro kwa kuanzisha kampeni ya kusambaza taarifa za uzushi. Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pompeo amesema serikali yake itajaribu kutumia kila njia kuhakikisha wanajeshi hao wanarejeshwa nyumbani.
Urusi, mshirika wa karibu wa Rais Maduro imemkosoa Trump na kuelezea kuwa hatua ya kipngozi huyo wa Marekani kukanusha kwake kuhusika sio ya kushawishi. Mwanasheria Mkuu wa Venezuela, Tarek William Saab amesema kiongozi wa upinzani, Juan Guaido, anayeungwa mkono na Marekani na zaidi ya nchi 50, alisaini mkataba wa Dola milioni 212 na "mamluki walioajiriwa" kwa kutumia fedha zilizotaifishwa na Marekani kutoka kwenye kampuni ya mafuta ya taifa ya PDVSA.
Watuhumiwa walisaini mkataba
Wakati huo huo, Luke Denman alisema jana kwamba amesaini mkataba na Jordan Goudreau, mmiliki wa kampuni ya usalama ya Florida ili kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa Caracas na kuipeleka ndege itakayomsafirisha Rais Maduro kwenda Marekani.
Hata hivyo, maafisa wa sheria wa Marekani wamesema Jordan, mwanajeshi mkongwe wa zamani wa kikosi maalum cha jeshi la Marekani, ambaye amedai kuhusika na jaribio hilo la Venezuela, anachunguzwa na shirikisho kwa kuuza silaha.
Kwa mujibu wa wanasheria hao, uchunguzi wa Jordan uko katika hatua za awali na haijafahamika kama atafunguliwa mashtaka. Mwezi Machi, Jordan alishtakiwa na serikali ya Trump kwa madai ya ugaidi yanayohusiana na biashara haramu ya dawa za kulevya.
(AFP, AP, Reuters)