1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yavishambulia vijiji vya Wakurdi Syria

Sylvia Mwehozi
19 Januari 2018

Kundi la wanamgambo wa Kikurdi la Syria YPG, limesema vikosi vya Uturuki vimerusha makombora karibu 70 na kuvilenga vijiji vya Wakurdi katika mkoa wa Afrin huko Kaskazini magharibi mwa Syria,

https://p.dw.com/p/2rAIC
Türkei Panzer in der syrischen Grenze
Picha: picture alliance/dpa/Zumapress/AA

Msemaji wa kundi la YPG Rojhat Roj ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mashambulizi hayo ya kutokea upande wa Uturuki yalianza usiku wa jana na kuendelea hadi asubuhi ya leo Ijumaa. Amesema yalikuwa mashambulizi makubwa tangu serikali ya Uturuki ilipotangaza kitisho cha kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya mkoa huo wa Wakurdi. Roj aliyekuwa akizungumza kutoka Afrin, amesema kundi la YPG litajibu kwa nguvu shambulio lolote katika mkoa huo.

Hayo yakijiri waziri wa ulinzi wa Uturuki amesema nchi yake haitarudi nyuma katika uamuzi wake wa kuanzisha mashambulizi dhidi ya eneo linalodhibitiwa na Wakurdi huko kaskazini Magharibi mwa Syria akisema kwamba mashambulizi yameanza moja kwa moja kwa jeshi la Uturuki kushambulia eneo hilo. Nurettin Canikli ameiambia televisheni ya Uturuki ya A Haber katika mahojiano kwamba wapiganaji wa Kikurdi wa Syria katika eneo la Afrin na wa maeneo mengine ni kitisho halisi kinachoongezeka kwa Uturuki. "Bila shaka aina hii ya operesheni ya kijeshi ni muhimu, ni operesheni ya kuvuka mipaka na inaendeshwa, tutafanya lolote linalowezekana ili kupunguza hasara iwezekanavyo," amesema waziri huyo. 

Türkei Verteidigungsminister Nurettin Canikli
waziri wa ulinzi wa Uturuki Nurettin CanikliPicha: imago/Depo Photos

Uturuki inalichukulia kundi la YPG kama utanuzi wa kundi la waasi la Kikurdi ambalo linapigana ndani ya Uturuki, kwahiyo inataka kuondoa kitisho chake na kuzuia uanzishaji wa ukanda wa Kikurdi kando ya mipaka yake. Kumekuwepo na idadi kubwa ya wanajeshi na mizinga kwenye mpaka wake katika wiki za karibuni. 

Syrien YPG Kämpfer
wapiganaji wa kundi la YPG la Syria Picha: Getty images/A. Sik

Hata hivyo Marekani imeunda uhusiano wa karibu na kundi la YPG kutokana na kuwa na maslahi sawa kwenye mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Waziri huyo wa ulinzi wa Uturuki anasema nchi yake imedhamiria kufanya mashambulizi makali katika mkoa wa Afrin na kwamba haitarudi nyuma katika uamuazi wake huo.

Hata hivyo hakusema lini operesheni hiyo itafanyika akiongeza kuwa mamlaka zinafanyia kazi wakati mzuri wa kufanya mashambulizi. Canikli amesema operesheni hiyo itaendeshwa na wapiganaji wa upinzani wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki kwa msaada wa vikosi vya Uturuki.

Na mashambulizi ya mabomu katika mji wa Kaskazini mashariki mwa Syria yaliyofanywa na waasi wanaoungwa mkono na Uturuki yamewaua angalau watu 14 katika hospitali ya wagonjwa wa akili. Mashambulizi hayo ya jana Alhamis katika mji wa Azaz kando ya mpaka wa Uturuki yamekuja baada ya Ankara kushambulia eneo la karibu la wakurdi la Afrin kwa siku tano mfululizo.

Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria lenye makao makuu nchini Uingereza limesema mabomu hayo yalirushwa na vikosi vya jeshi la Kidemokrasia la Syria, muungano wa kijeshi unaoungwa mkono na Marekani ukitawaliwa zaidi na kikundi cha ulinzi wa Wakurdi YPG.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/AP/reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman