1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatishia kusitisha makubaliano kuhusu wakimbizi

Caro Robi1 Agosti 2016

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema Uturuki itajiondoa kutoka makubaliano iliyofikia na Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi iwapo Umoja huo hautaruhusu raia wake kuingia katika nchi zao bila ya visa.

https://p.dw.com/p/1JZV9
Picha: picture alliance/AP Photo/A. Unal

Cavusoglu amesema Uturuki itajiondoa kutoka makubaliano hayo iwapo raia wake hawataruhusiwa kuingia nchi za Umoja wa Ulaya bila ya visa ifikapo mwezi Oktoba.

Mwezi Machi mwaka huu, Uturuki na Umoja wa Ulaya zilifikia makubaliano ya kuzuia mmiminiko wa wakimbizi, ambapo miongoni mwa ahadi Uturuki iliahidiwa ni kuharakishwa kwa mazungumzo kuhusu nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya na raia wake kuruhusiwa kuingia bila ya visa katika nchi za Umoja wa Ulaya.

EU yataka Uturuki kuheshimu sheria kwanza

Kamishna wa Umoja wa Ulaya Günther Oettinger amesema haoni Umoja huo ukiridhia raia wa Uturuki kuingia katika nchi hizo kufuatia msako mkubwa unaoendelea Uturuki baada ya jaribio la mapinduzi yaliyotibuka. Kumekuwa na kamata kamata nchini Uturuki tangu jaribio hilo la mapinduzi mnamo tarehe 15 mwezi uliopita.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AA/A. Izgi

Zaidi ya watu 60,000 wamekamatwa wakiwemo maelfu ya wanajeshi, polisi, wanahabari, walimu, maafisa wa idara ya mahakama na wafanyakazi wa umma wanazuiwa kwa shutuma za kuhusika katika njama hiyo ya kuipindua serikali inayodaiwa kupangwa na hasimu wa Rais Erdogan aliye uhamishoni Marekani Sheikh Fethullah Gulen.

Shirika la habari la Uturuki Anadolu leo limeripoti kikosi maalum cha jeshi limewakamata makomando 11 wa kijeshi waliohusika katika njama ya kumkamata Rais Erdogan katika eneo la Marmaris wakati wa mapinduzi hayo yaliyotibuka.

Jumuiya ya kimataifa imeelezea wasiwasi wake kuhusu kukamatwa na kuzuiwa kwa maelfu ya watu Uturuki. Marekani na Umoja wa Ulaya zimeuonya utawala wa Erdogan kuheshimu sheria na kuzingatia haki za binadamu.

Uturuki imesema mara kwa mara ina nia ya kuanzisha tena sheria ya hukumu ya kifo kuwaadhibu waliohusika katika njama ya kuipindua serikali.

Huku hayo yakijiri, hapo jana maelfu ya watu walihudhuria maandamano makubwa katika mji wa Cologne, Ujerumani kuunga mkono utawala wa Rais Erdogan. Zaidi ya waturuki 40,000 wanaoishi Ujerumani walijitokeza kuhudhuria maandamano hayo.

Waturuki waandamana Ujerumani

Waandalizi wa maandamano hayo wamesema maandamo hayo hayakuwa tu ya kumuunga mkono Erdogan, bali ya kuunga mkono demokrasia.

Raia wa Uturuki wakiandamana Cologne kumuunga mkono Erdogan
Raia wa Uturuki wakiandamana Cologne kumuunga mkono ErdoganPicha: picture alliance/AP Photo/M. Meissner

Kulikuwa pia na maandamano sambamba katika mji huo wa Cologne na maelfu ya polisi walipiga doria kuhakikisha usalama na kuzuia mkwaruzano kati ya makundi hayo hasimu. Kuna takriban waturuki milioni tatu wanaoishi Ujerumani. Rais Erdogan alitarajiwa kuwahutubia waandamanaji hao kupitia mawasiliano ya kurushwa moja kwa moja kupitia video lakini polisi ilipiga marufuku hatua hiyo.

Kufuatia marufuku hiyo, balozi wa Ujerumani nchini Uturuki ametakiwa kufika mbele ya wizara ya mambo ya nje ya Uturuki leo mchana. Uturuki pia inaitaka Ujerumani kuwarejesha nyumbani wafuasi wa Gulen wanaoishi Ujerumani.

Wakati huo huo, viongozi wa kijeshi na wa kisiasa wa Uturuki na Marekani wanakutana leo mjini Ankara katika mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja kati yao tangu jaribio la mapinduzi. Uhusiano kati ya Uturuki na Marekani umekuwa si mzuri tangu njama hiyo, kukiwa na madai kutoka Uturuki kuwa Marekani ilihusika katika jaribio hilo.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dw Eng

Mhariri: Josephat Charo