Uturuki yakiri kukutana na Urusi na Iran kuijadili Syria
6 Desemba 2024Chanzo kutoka wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imesema Waziri Hakan Fidan atakutana na mawaziri wenzake wa Urusi na Iran kwa mkutano chini ya mchakato wa Astana, kandokando na kongamano linalofanyika mjini Doha, kesho Jumamosi.
Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa mkutano huo utafanyika kati ya Uturuki, inayounga mkono baadhi ya makundi ya waasi nchini Syria na washirika wa Damascus, Iran na Urusi.
Umoja wa Mataifa watoa wito wa kupunguza uhasama Syria
Mchakato unaojulikana kama Astana, unaozihusisha nchi hizo tatu, ulianzishwa na Kazakhstan mwaka 2017 kwa lengo la kupata suluhisho la kisiasa kwa vita nchini Syria, vilivyoibuka upya baada ya kundi la waasi wenye itikadi kali za dini kufanya mashambulizi ya ghafla ikivilenga vikosi vya usalama vya serikali.
Qatar ambayo mwanzoni iliunga mkono waasi baada ya serikali ya Rais Bashar al-Assad kuzima maandamano ya amani mwaka 2011, imesalia kuwa mkosoaji mkubwa wa Assad japo inatoa wito wa kumalizwa kwa vita hivyo kwa njia ya mazungumzo.