1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatangaza kutuma wanajeshi wake Kosovo kutuliza hali

3 Juni 2023

Wizara ya ulinzi ya Uturuki imetangaza kutuma wanajeshi wake Kaskazini mwa Kosovo ikijibu ombi la Jumuiya ya kujihami NATO kuitisha wanajeshi zaidi wa kutuliza machafuko katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4S9uv
Kosovo | KFOR Friedensmission
Picha: Erkin Keci/AA/picture alliance

Wizara ya ulinzi ilisema wanajeshi wake watajiunga na Ujumbe wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Kosovo  - KFOR bila ya kufafanua ni wanajeshi wangapi hasa watakaopelekwa nchini humo. 

Hata hivyo mapema wiki hii NATO ilisema inapanga kuwapeleka wanajeshi 700 ili kulinda amani Kaskazini mwa Kosovo baada ya wanajeshi wake 30 kujeruhiwa katika makabiliano kati ya polisi wa kosovo na watu wa kabila la serbs. 

Uturuki kupitia taarifa yake imezitaka pande mbili kuchukua hatua za kutuliza mvutano unaohatarisha usalama na udhabiti wa kikanda. Zoezi la kuwapeleka wanajeshi linatarajiwa kuanza kesho Jumapili hadi Jumatatu. 

Machafuko yalianza wakati kabila la Serb linalochangia asilimia 6 ya idadi Jumla ya watu wa Kosovo liliposusia uchaguzi  wa serikali za mitaa uliokuwa na utata uliofanyika mwezi Aprili, katika miji ya Kaskazini linakopatikana kwa wingi na kutoa nafasi kwa kabila la Albania kuchukua udhibiti wa mabaraza ya jiji. 

Waserbia wengi wanataka  kuondolewa kwa vikosi vya polisi na ma meya wa kabila la Albania ambao hawawaoni kama wawakilishi wao.